>

HONGERA KOMBA,WENGINE WAJIFUNZE

KWA ambalo limetokea kwa waamuzi wa Tanzania bado kuna jambo la kujifunza ili wakati ujao orodha ya majina ya waamuzi ambao watapewa nafasi ya kuchezesha mashindano ya kimataifa izidi kuongezeka.
Mwamuzi Mtanzania, Frank Komba ni yeye pekee ambaye ameweza kupenya kwenye orodha hivyo katika hilo kuna jambo la kujifunza.

Kwa Komba kuteuliwa na CAF kuwa miongoni mwa Waamuzi watakaochezesha michuano ya AFCON inayotarajiwa kuanza mwezi Januari ni hatua kubwa na inahitaji pongezi kwake kwa kuwa sio hatua nyepesi.

Ukitazama ile orodha ya waamuzi ambao wameteuliwa utagundua kwamba wapo waamuzi wengine kutoka nchi mbalimbali wameteuliwa zaidi ya wawili.

Nchi jirani na sisi na ndugu zetu ambao ni Kenya wao pia wametoa waamuzi ambao watachezesha Afcon mwakani.

Itakuwa ni nchini Cameroon mashindano hayo makubwa na yanayofuatiliwa na wengi yanatarajiwa kufanyika.

Kenya ni majina mawili ya waamuzi yamepenya katika hilo wameonekana kwamba wamepiga hatua lakini bado kuna jambo la kujifunza.

Morocco wanaonekana wametia fora kwenye orodha ya waamuzi ambapo mpaka sasa orodha inaonyesha kwamba kuna waamuzi saba ambao wametoka huko.

Maana yake ni kwamba wale ambao wanatoka huko wanapenda kufuata sheria 17 na kufanya vizuri katika mashindano yote wanayopewa kuyasimamia.

Basi ni wakati wa waamuzi wa Tanzania kuweka kando yale ambayo yamekuwa yakiwafanya washindwe kufanya vizuri hivyo ni muda wa kuboresha sasa na kufanya vizuri kwenye mechi za Ligi Kuu Bara pamoja na mashindano mengine ambayo yanatazamwa.

Komba amefungua njia wengine kuna jambo la kujifunza.