WAKATI mwingine sasa kwenye ulimwengu wa soka Bongo ni muda wa usajili wa dirisha dogo ambapo ni fursa kwa timu kuboresha pale ambapo wameona kuna matatizo.
Usajili wa dirisha dogo huwa hauwi mkubwa sana kwa kuwa ni nafasi chache ambazo zinahitajika kufanyiwa kazi kulingana na ripoti ya benchi la ufundi.
Jambo la msingi ambalo linapaswa kuzingatiwa katika usajili ambao unafanywa ni kufuata ripoti ya mwalimu, yeye ndiye ambaye anajua kwamba anahitaji aina gani ya wachezaji kwenye kikosi chake.
Wapo wale ambao watafanya usajili kwa kufuata mahitaji yao hilo lipo wazi kwa kuwa ni mambo ambayo yapo kwenye soka letu la Bongo. Zama hizo muda wake umekwisha halipaswi lipewe nafasi kwa sasa.
Muda wa kufanya kazi kwa utaalamu na kufuata taaluma ya kazi ya mpira ni sasa. Soka letu linazidi kukua kwa kasi ikiwa masuala ya kufanya maamuzi kwa kuwa wewe ni kiongozi haileti picha nzuri kwa afya ya soka letu.
Timu zote ambazo zitafanya usajili kwa mapendekezo yao binafsi wakati wa kujua masuala hayo yanakuja, mchezo wa mpira hauhitaji mambo mengi zaidi ya vitendo na data ambazo zinaongea ukweli muda wote.
Ndani ya dakika 90 ni muda sahihi uwanjani ambao utatosha kuaminisha mashabiki na wanachama wa timu kwamba huyo aliyeletwa ndani kucheza ni pendekezo la kocha ama kiongozi.
Sababu moja kubwa itakayofanya atambulike kwamba alisajiliwa kwa presha ama chaguo la kiongozi ni muda wake atakaoutumia ndani ya uwanja na kile ambacho atakionyesha pia pale atakapopata muda.
Ipo wazi kwamba kuna wale wachezaji ambao walipata nafasi ya kusajiliwa kwa msimu wa 2020/21 ndani ya timu mbalimbali hawakuwa na nafasi kwenye timu zao mpaka msimu unaisha.
Namba hazidanganyi kwani wapo wachezaji ambao wamecheza mechi 10 na zote walianzia benchi na hata pale ambapo walianza kikosi cha kwanza hawakumaliza dakika zote 90.
Kasumba ya kufanya usajili kwa presha imekuwa ikiwafanya wachezaji kushindwa kupata nafasi kwenye timu ambazo wanakwenda na kuishia kujenga urafiki na benchi.
Hamna namna maisha ya soka lazima yaendelee mchezaji mmoja kutoka na kwenda kwenye timu nyingine ni muda sahihi wa kila mchezaji ambaye anakwenda kuanza maisha mapya.
Imani yangu ni kwamba mpaka pale dirisha la usajili litakapofungwa kila kitu kitakuwa kimekwenda sawa ndani ya timu zote kuanzia zile za Ligi Daraja la Kwanza, Daraja la Pili,Ligi ya Wanawake pamoja na zile zinazoshiriki Ligi Kuu Bara.
Pia kwa waamuzi ambao wataoewa nafasi ya kuweza kuchezesha mechi za ligi ni wakati wao kufuata sheria 17 ili waweze kwenda sawa na kasi ya mchezo.
Ngoma nzito sana kwa waamuzi hasa kutokana na kila mmoja kuwa na lake kuhusu waamuzi, ukweli ni kwamba maendeleo ya mpira wetu yanahitaji usimamizi mzuri wa sheria 17 ambazo zinafanywa na waamuzi.
Ikawe hivyo kwa mechi zijazo waamuzi kuacha kuegemea kwenye kivuli cha makosa ya kawaida ikiwa kila siku itakuwa kawaida hii ni haileti picha nzuri kwa soka letu la Tanzania.
Kila kitu kinawezekana ikiwa mipango makini itapangwa ikawe hivyo kwa waamuzi na wachezaji watakaopata nafasi kwenye maisha mapya ndani ya timu mpya.