>

MAJEMBE MAPYA YANGA KUANZA KAZI

RASMI uongozi wa Yanga umefunguka kuwa kuna uwezekano mkubwa wa wachezaji wapya watakaosajiliwa na timu hiyo katika dirisha hili dogo la usajili kutumika katika michuano ya Kombe la Mapinduzi itayoanza kutimua vumbi Januari visiwani Zanzibar.


Yanga katika dirisha hili dogo la usajili 
wanahusishwa kwa karibu na baadhi ya wachezaji akiwemo mshambuliaji Jean Marc Makusu anayekipiga DC Motema Pembe na kiungo mshambuliaji Fabrice Ngoma anayekipiga Raja Casablanca ya Morroco.

Pia wanatajwa kumalizana na winga wa Biashara United, Dennis Nkane ambaye ameletwa duniani 2003.

Ofisa Habari wa Yanga, Hassan Bumbuli aliweka wazi kuwa timu hiyo itafanya usajili wa wachezaji kupitia dirisha hili dogo la usajili ambapo katika usajili huo wapo ambao watatumika katika michuano ya Mapinduzi na wengine hawatatumika katika michuano hiyo kulingana na matakwa ya timu.

“Yanga kupitia dirisha dogo la usajili lazima tutafanya usajili wa wachezaji ambapo mara baada ya kumalizika kwa mchezo wetu wa ligi dhidi ya Biashara United, basi tutaelekea katika Kombe la Mapinduzi ambapo kuna wachezaji ambao tutawasajili wataitumikia timu katika michuano.


“Yanga kwa sasa kuna wachezaji 
wengi ambao ni majeruhi kama Yacouba Songne, Yusuph Athuman, Kibwana Shomari hivyo lazima kufanyike usajili kwa baadhi ya maeneo kulingana na wapo ambao watakosekana kwa muda mrefu na hivi karibuni maingizo mapya yatajulikana.


“Wachezaji wote ambao watasajiliwa 
watajulikana na uongozi wa Yanga na benchi la ufundi ndio unafahamu ila hao ambao unawasikia sio rasmi kutoka kwetu,” alisema Bumbuli.