>

WAAMUZI MSIJIKAUSHE,KUTOCHAGULIWA AFCON NI TATIZO LENU KUBWA

IMETOKA orodha ya waamuzi waliopata nafasi ya kuchezesha michuano ya Afcon lakini kwa Tanzania hakuna ambaye amechaguliwa.

Waamuzi waliotaganzwa kuchezesha michuano hiyo, wapo kutoka karibu kila nchi hata zile za jirani kama Uganda na Rwanda lakini Tanzania haina nafasi.

Nasema Tanzania haina nafasi baada ya kutopata nafasi hata ya mwamuzi mmoja aliyeteuliwa katika hatua hiyo kupata nafasi ya kuchezesha michuano hiyo mikubwa barani Afrika.

Kukosekana kwa mwamuzi hata mmoja wa Tanzania katika michuano hiyo, si jambo la kuliachia lipite tu kwa kuwa tunaliona ni kama jambo la kawaida.

Kutopata kwa nafasi ni wazi kuwa tunakosa waamuzi wenye viwango sahihi vinavyoweza kuwafanya wapate nafasi ya kuchezesha michuano mikubwa ya Afcon.

Hii si mara ya kwanza au ya pili na hili limekuwa likitokana na uduni wa viwango vya waamuzi wetu na suala la uchezeshaji wao katika mechi mbalimbali na hasa za Ligi Kuu au Daraja la kwanza imekuwa ni sehemu ya kuonyesha kiwango chao.

Sote tunajua kumekuwa na malalamiko makubwa ya viwango vya waamuzi na suala la “Makosa ya Kibinadamu” limekuwa ngao ya mauovu ya waamuzi wengi.

Bahati mbaya, hatuwezi kuwaambia sana ukweli kwa kuwa ushabiki wa timu kubwa wa Yanga na Simba unatufunika macho kwa kuwa anayekosea huku atatetewa na wale, na anayekosea kule anatetewa na hawa.

Niwakumbusha, Tanzania leo inaonyesha ligi yake kuwa moja ya ligi bora zaidi barani Afrika, si jambo dogo. Sasa kama ligi iliyo katika 10 bora, vipi inashindwa kuwa na mwamuzi hata mmoja anayechezesha Afcon.

Hapa unaanza kuona tofauti na maji na mafuta na bila shaka, inaonyesha kiasi gani kiwango cha soka letu kinavyoaacha waamuzi nyuma.

Wakati huu tulistahili kuwa na waamuzi ambao wangepata nafasi katika Afcon ikiwa ni sehemu ya mapinduzi ya ubora. Tunazungumzia viwanjani, maana yake waamuzi wanahusika na haiwezekani mwamuzi hadi ya ligi ya Rwanda au Burundi atambe na kuwa mwamuzi bora kuzidi wa Tanzania!

Waamuzi mnajisikiaje? Walimu wao wanajisikiaje? Bahati mbaya watu hawajataka kulizungumzia kwa kina suala hilo. Hilo wanaliona kwa kuwa ni waamuzi wala hakuna tatizo lolote lakini ukweli halisi si jambo sahihi hata kidogo.

Kwanza linatuonyesha kweli kuna walakini katika suala la ubora wa waamuzi na wakubali sasa, wasikatae kama ambavyo imekuwa ikionekana kama wanaonewa sana. Kama wangekuwa bora tungewaona katika ubora wa kiwango cha Afrika.

Hawapo Afcon hawana ubora wa kiwango cha Afrika na wanapaswa kukiri katika hili na kujiimarisha. Bila ya ubishi wanaokwenda Afcon wanakuwa ni cream ya Afrika na sisi hatuna uwezo wa kuwa nayo kwa sasa. Hivyo mpango mkakati uanzie katika kamati ya waamuzi.

TFF na Bodi ya Ligi, wamechangia sana kuwa na waamuzi bora. Wanatakiwa kusimamia kwa ufasaha haswa kupitia kama ya waamuzi kuhusiana na suala la ubora wa waamuzi, ili wasiendelee kutuangusha na kututia aibu.

Inawezekana pia kusiwe na mabadilio ya haraka ya viwango kwa kuwa waamuzi hawataki kuambiwa kuhusiana na kiwango duni, kila wanapokoselewa mara zote wanaona wanaonewa, nah ii huwafanya wabaki na kiwango chao cha siku zote.

Siamini kama Tanzania tunaweza vitu vingi ana na mabadiliko yamekuwa makubwa katika soka halafu litushinde hili la waamuzi ndio maana nikawashauri TFF na TPLG, walisimamie hili kwa ukaribu zaidi na viongozi wa klabu waachane na masuala ya kuwahonga waamuzi maana ndio wanafanya uwekezwaji mkubwa uhamie uhamie katika majungu na fitna badala ya uhalisia na usahihi.