>

YANGA:IHEFU NI BORA KULIKO SIMBA

UONGOZI wa Yanga umeweka wazi kuwa mchezo wa leo dhidi ya Ihefu ambao ni wa Kombe la Shirikisho ni bora kuliko ule wa Simba uliochezwa Jumamosi, Uwanja wa Mkapa na ngoma kukamilika kwa sare ya bila kufungana.

Thabit Kandoro,Mkurugenzi wa Mashindano ndani ya Yanga amesema kuwa wanakazi kubwa ya kufanya mbele ya Ihefu FC kwenye mchezo wa raundi ya tatu, Uwanja wa Mkapa.

Kandoro amesema:“Hatukufanikiwa kile ambacho tulikuwa tumekipanga kwenye mchezo wetu dhidi ya Simba lakini huo ni mchezo tumepata alama moja tunaongoza ligi na sasa  tunakwenda kwenye mchezo muhimu zaidi.

“Mchezo wetu dhidi ya Ihefu ni muhimu zaidi kwa sababu FA ni mchezo ambao ukifungwa unatoka tofauti na mchezo wa ligi ambao unaweza ukafungwa kisha ukajiokoa wakati ujao lakini mchezo wa FA ukipoteza unapotezwa.

“Timu imerejea kambini kujiandaa kwa ajili ya mchezo wetu dhidi ya Ihefu na majeruhi ni mmoja tu ambaye ni Yacouba Songne wengine wote wapo vizuri tunashukuru tunakwenda mwisho wa mwaka tukiwa na majeruhi mmoja.

“Hatumuangalii Ihefu kama Ligi Daraja la Kwanza tunajua kwamba ni moja ya timu bora kutoka nyanda za juu, tulicheza nayo kwenye ligi msimu uliopita na tuliweza kushinda pointi sita lakini hatuwabezi,” alisema Kandoro.