MSHAMBULIAJI wa Barcelona, Sergio Aguero mwenye miaka 33 ametangaza kustaafu soka kwa wakati huu kutokana na tatizo la moyo na amesema kuwa maamuzi hayo ni kwa ajili ya afya.
Aguero alianza kupata maumivu katika mchezo uliokamilka kwa sare ya kufungana bao mojamoja kati ya Barcelona dhidi ya Alaves ilikuwa ni Oktoba 2021.
Ikumbukwe kwamba Aguero alijiunga na Barcelona msimu huu bure kwa dili la miaka miwili akitokea Klabu ya Manchester City ambapo huko aliweka rekodi ya kuwa mzee wa kutupia tu katika misimu 10 ambayo amecheza.
City ilipata saini ya Aguero 2011 akitokea Klabu ya Atletico Madrid na aliweza kufunga bao la maajabu katika msimu 2011/12 na kuipa timu hiyo taji la kwanza la Ligi Kuu England.
Jumla alipachika mabao 260 katika timu na alicheza jumla ya mechi 390, ni mataji matano ya Ligi Kuu England alitwaa, mataji sita ya League Cup.
Aguero amesema:”Huu mkutano ni maalumu kwa ajili ya kuwasilisha ujumbe kwamba nimeamua kusimama kucheza mpira. Ni wakati mgumu na maamuzi ambayo nimeyachukua ni kwa ajili ya afya yangu hii ni sababu kubwa,”.