>

SIMBA NA YANGA WAMEVUNA WALICHOKIPANDA

KUSHINDWA kutumia makosa ambayo mpinzani wako anafanya kwenye mpira ni sababu namba moja itakayofanya timu ishindwe kupata matokeo.

Na yule ambaye hatafanya makosa ana uhakika mkubwa wa kupata kile ambacho anastahili hivyo ipo wazi kwamba matokeo hayapaswi kubebwa na mashabiki kwenye mifuko yao.

Baada ya Kariakoo Dabi kukamilika Uwanja wa Mkapa tumeona baadhi ya mashabiki wakilalamika huku wengine wakifurahi kwa kupata pointi moja yote ni matokeo ya maandalizi.

Jambo kubwa na muhimu la kufanya kwa wakati huu ni maandalizi mazuri kwa ajili ya mechi zijazo kwa kuwa mwisho wa kazi moja ni mwanzo wa kazi nyingine ngumu.

Napenda pia kuwapa pongezi mashabiki ambao walijitokeza kushangilia timu zao hilo ni jambo la msingi kwa kuwa mpira unaishi pia kwa uwepo wa mashabiki.

Imani yangu ni kwamba kuna jambo mmejifunza kwa wale ambao mlibeba matokeo yenu mfukoni na kuingia nayo Uwanja wa Mkapa.

Wachezaji pia nimeona namna ambavyo walicheza kwa nidhamu kubwa katika kutimiza majukumu yao nao pia wanastahili pongezi.

Makosa ambayo wameyafanya kisha wapinzani wao wakashindwa kuyatumia wanakazi ya kuweza kufanyia maboresho wakati ujao ili kuwa imara zaidi.

Niliweka wazi kwamba kuna ulazima wa wachezaji kufanya maandalizi mazuri na kuwa vizuri kisaikolojia kwa ajili ya matokeo ambayo yatapatikana baadaa ya dakika 90.

Imekuwa hivyo na tumeona makosa ambayo yamefanyika ni yale ya kawaida hilo haliwezi kukwepeka na ipo hivyo siku zote.

Ukiachana na mchezo wa Simba na Yanga kwa sasa tunaona kwamba ni raundi ya tatu ya Kombe la Shirikisho ambapo timu zinaendelea kupambana kusaka ushindi.

Hivyo ukweli ni kwamba Simba na Yanga wamevuna kile ambacho wamekipanda na tumeona wazawa nao wamekuwa imara kuonyesha kile ambacho wanacho kwenye miguu yao.

Katika  hili ni muhimu wachezaji kutambua kwamba malengo ya timu yapo ili yaweze kutimizwa na wanaopaswa kuyatimiza ni wachezaji wenyewe.

Kwa namna yoyote ile kwenye mashindano ambayo timu zinashiriki hesabu kubwa ni kupata ushindi hivyo ili kushinda ni muhimu kuweza kupambana kupata kile ambacho.

Haya ni mashindano makubwa na yanahitaji kupewa kipaumbele kwa kila timu shiriki ili kupata ushindi hasa ukizingatia kwamba kuna zawadi pamoja na kuweza kushiriki katika mashindano ya kimataifa.

Hili ni daraja kwa timu shiriki kuweza kuibeba nchi kimataifa na ili iwezekane kuwa hapo lazima kupambana kwa hali na mali katika kusaka ushindi.

Waamuzi ambao watapewa majukumu ya kusimamia mashindano haya kazi yao iwe moja kufuata sheria 17 za soka kwa kuwa wakifanya hivyo kila kitu kitakwenda sawa.

Yale malalamiko ambayo yamekuwa yakitokea kwenye mechi za ligi basi yanapaswa yapunguzwe na kufanyiwa kazi kabisa huku kwenye kombe la Shirikisho.

Basi kila la kheri wachezaji na waamuzi ambao wanasimamia mashindano haya kila kitu kinawezekana.