>

MTIBWA SUGAR YASHINDA MARA YA KWANZA KWENYE LIGI,NDEMLA ATUPIA

KIKOSI cha Mtibwa Sugar kimeweza kuonja ladha ya ushindi kwa mara ya kwanza ndani ya Ligi Kuu Bara msimu wa 2021/22 baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Biashara United.

Mchezo huo wa nane kwa Mtibwa Sugar ulichezwa Uwanja wa Manungu, Desemba 12 na Mtibwa Sugar iliweza kushinda kupitia kwa Nzigamasabo Stive dakika ya 13 kwa mkwaju wa penalti na Said Ndemla alipachika bao dakika ya 73.

Watupiaji wote ndani ya Mtibwa Sugar wanafunga kwa mara ya kwanza wakiwa na jezi za Mtibwa Sugar ambapo Stive yeye alikuwa akikipiga Namungo FC na Ndemla ameibuka hapo akitokea ndani ya kikosi cha Simba.

Ushindi huo unaifanya Mtiwa Sugar kuambulia pointi tatu kwa mara ya kwanza kwa kuwa walikuwa wamecheza mechi 7 bila kushinda na walikuwa wamelazimisha sare mbili na kufungwa mechi tano.

Kibindoni wana pointi tano wakiwa nafasi ya 15 wakipanda kwa nafasi moja kutoka ile ya 16 ambayo walijijengea huko kwa muda na nafasi ya 16 ipo mikononi mwa Geita Gold yenye pointi tano tofauti ikiwa ni mabao ya kufunga na kufungwa.

Mtibwa Sugar imefunga mabao manne huku Geita Gold ikiwa imefunga mabao matano kwa upande wa mabao ya kufungwa Mtibwa imefungwa mabao nane na Geita Gold mabao 11.