KIUNGO mkabaji wa Yanga, Mganda, Khalid Aucho, amesema kuwa hataki kuuzungumzia mchezo wa Kariakoo Dabi na kikubwa yeye anataka kuonyesha ubora na uwezo wake uwanjani kesho Jumamosi.
Hiyo ni katika kuelekea mchezo ujao wa dabi utakaozikutanisha Simba na Yanga kwenye Uwanja wa Mkapa jijini Dar.
Mganda huyo alikuwa nje ya uwanja kwa wiki moja akisumbuliwa na majeraha yaliyomsaba- bishia kukosa michezo miwili dhidi ya Ruvu Shooting na Namungo FC lakini sasa yupo fiti kuivaa Simba.
Akizungumza na Championi Ijumaa, Aucho alisema kuwa yeye siyo muongeaji mara nyingi anapenda kufanya vitu kwa vitendo uwanjani.
Aucho alisema kuwa anaamini kiwango chake ndani ya uwanja kwa kushirikiana na wachezaji wenzake
watapata matokeo mazuri.
“Naamini mashabiki wa Yanga wana imani na timu yao kutokana na ubora wa kikosi chetu ambacho hakijapoteza mchezo wowote wa ligi. “Niwatake mashabiki wa Yanga kujitokeza kwa wingi kwa ajili ya kutusapoti uwanjani ili tupate matokeo mazuri.
“Mimi siyo muongeaji sana, mimi napenda kufanya kazi kwa vitendo, hivyo tukutane Desemba 11 katika Uwanja wa
Mkapa,” alisema Aucho.