RASMI Kocha Mkuu wa Simba, Mhispania, Franco Pablo, amemuondoa mshambuliaji Chris Mugalu na kiungo
mkabaji, Taddeo Lwanga katika mfumo wake kuelekea Kariakoo Dabi itakayowakutanisha Simba dhidi Yanga
kesho Jumamosi kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar.
Nyota hao wote wapo nje ya uwanja kwa muda mrefu wakiuguza majeraha ya goti wote wawili.
Mmoja wa mabosi kutoka ndani ya benchi la ufundi la timu hiyo, ameliambia Championi Ijumaa kuwa wachezaji hao licha ya kupona na kuanza mazoezi lakini hawapo katika mipango ya kocha katika kuelekea dabi.
Bosi huyo alisema kuwa kocha huyo tayari amewaondoa katika mfumo wake atakaotumia katika pambano hilo.
“Lwanga na Mugalu wote walianza mazoezi lakini kocha kawaangalia na kuchukua maamuzi ya kuwaondoa kabisa
katika mipango yake.
“Wamepona lakini kocha baada ya kuwaona uwanjani alibaini wamekosa fitinesi ya kutosha itakayowafanya
kucheza mchezo huo,” alisema bosi huyo.
Akizungumzia hilo, Kaimu OfisaHabari wa Simba, Ally Shatry, alisema kuwa wachezaji hao wamepona, lakini
suala la kucheza lipo kwa kocha.