NASREDDINE Nabi, Kocha Mkuu wa Yanga ameweka wazi kuwa yeye ni mtu wa mpira na hapendi manenomaneno.
Timu hiyo kwa sasa inaendelea na maandalizi kuelekea katika mchezo wa Kariakoo Dabi ambao unasubiriwa kwa shauku kubwa na mashabiki pamoja na wadau wa mpira.
Yanga iliyo nafasi ya kwanza na pointi 19 inatarajiwa kumenyana na Simba iliyo nafasi ya pili na pointi 17 kibindoni na zote zimecheza mechi 7.
Raia huyo wa Tunisia ameweka wazi kwamba anatambua mchezo huo utakuwa na ushindani mkubwa lakini wapo tayari kupata ushindi.
“Mimi ni mtu wa mpira na sipendelei sana manenomaneno zaidi ya kufanya kazi, unajua kila mtu anafanya vizuri katika kitu ambacho anakipenda na anakijua hivyo mimi ni mtu wa mpira.
“Wapinzani wetu nawaheshimu na nimewaona namna ambavyo wanacheza ni jambo la kusubiri na kuona itakuaje lakini ninachoweza kusema ni kwamba tupo tayari, ” amesema.
Desemba 11,2021, Uwanja wa Mkapa mchezo huo unatarajiwa kuchezwa majira ya saa 11:00 jioni ambapo Simba watakuwa wenyeji kwenye mchezo huo.