NYOTA HAWA WATAPEWA MAJUKUMU YA MIPIRA ILIYOKUFA

  FUKUTO kwenye vichwa vya mashabiki wa soka Bongo linahesabu saa tu kwa sasa kabla ya Desemba 11,2021 kuwadia na kushuhudia Kariakoo Dabi.

  Itakuwa ni Simba v Yanga, Uwanja wa Mkapa ambapo utakuwa ni mchezo wa kwanza kwenye ligi kwa msimu huu na kuna wachezaji ambao wao wanasubiri kutimiza majukumu yao ya kutumia mipira ile iliyokufa ikiwa ni penalti, faulo pamoja na ile ya kurushwa kuelekea kwa wapinzani wao.

  Hapa tunakuletea nyota wa timu hizi mbili ambao majukumu hayo yapo mikononi mwao namna hii:-

  Rally Bwalya

  Kwenye mchezo dhidi ya Namungo FC uliochezwa Uwanja wa Mkapa,Novemba 3, Bwalya alipiga jumla ya faulo saba na kona mbili huku mguu wake wenye nguvu ni ule wa kushoto ambao anapenda kuutumia.

  Pia ana bao moja ambalo alifunga mbele ya Polisi Tanzania, Uwanja wa Mkapa Oktoba 27 na ubao ulisoma Simba 1-0 Polisi Tanzania.

  Bernard Morrison

  Kwenye mchezo dhidi ya Namungo FC alipiga jumla ya kona nne na faulo moja Uwanja wa Mkapa ilikuwa Novemba 3. Pia mbele ya Ruvu Shooting alipiga jumla ya kona 8 ilikuwa ni Novemba 19,2021 katika mchezo uliochezwa Uwanja wa CCM Kirumba na alitoa pasi ya bao ambalo lilifungwa na Meddie Kagere kwa pigo la kona.

  John Bocco

  Nahodha ambaye anapambana kutetea kiatu chake cha ufungaji bora na msimu uliopita alifunga mabao 16 na pasi mbili. Msimu huu wa 2021/22 mambo bado kwake.

  Akiwa amecheza mechi sita kati ya saba na kuyeyusha dakika 387 bado hajafunga bao.Alipewa jukumu la kupiga penalti kwenye mchezo dhidi ya Biashara United, haikuwa bahati kwake kwa kuwa mlinda mlango James Ssetuba alitimiza majukumu yake kwa kuipangua penalti hiyo.

  Mzamiru Yassin

  Mguu wake anaopenda kuutumia ni ule wa kulia akiwa amecheza mechi tano na kutumia dakika 259 amefunga bao moja akitumia pasi ya Bernard Morrison kwa mpira wa faulo alipowafunga Geita Gold. Licha ya kwamba hajafunga kwa njia ya faulo lakini wakati mwingine amekuwa akipewa majukumu ya kupiga faulo.

  Mohamed Hussein na Kapombe

  Mrusha mipira ya Simba pale inapotoka nje asilimia kubwa huwa anakuwa ni Zimbwe na wakati mwingine wanasaidiana na mshikaji wake Shomari Kapombe.Hivyo Desemba 11 watakuwa na jukumu la kurusha mipira kuelekea lango la Yanga.

  Yanga

  Said Ntibanzokiza

  Mtaalamu wa mipira iliyokufa ndani ya Yanga ni mwamba Ntibanzokiza ambapo mabao yake yote mawili yametokana na mipira ya adhabu.

  Alifunga bao la kwanza mbele ya Namungo FC kwa mkwaju wa penalti na bao la pili alifunga mbele ya Mbeya Kwanza ilikuwa ni kwa pigo la faulo akiwa nje kidogo ya 18.

  Djuma Shaban

  Bao lake moja kibindoni aliwatungua Ruvu Shooting ilikuwa Uwanja wa Mkapa kwa mkwaju wa penalti. Pia nyota huyu amekuwa na kazi ya kurusha mipira hivyo atakuwa na jukumu la kupeleka mashambulizi kwa Simba mwanzo mwisho.

  Fiston Mayele

  Mwamba huyu mwenye mabao matatu na pasi moja ya mwisho amekuwa akitumiwa kupiga faulo fupi kwenye mechi za ligi na anapewa nafasi ya kuweza kufanya hivyo mbele ya Simba ikiwa ataanza kikosi cha kwanza.

  Feisal Salum

  Simba wanamtambua kuwa kila anapokutana nao huwa anakuwa hana shughuli ndogo hasa kwa mishuti yake inayokera. Kutokana na uwezo wa kupiga mashuti ya mbali na yenye ujazo anapewa nafasi ya kuweza kupiga mipira iliyokufa.

  Akiwa na mabao matatu ndani ya ligi ni bao moja pekee alifunga akiwa ndani ya 18 ilikuwa mbele ya Kagera  Sugar lakini mbele ya Ruvu Shooting na KMC yote ilikuwa ni nje ya 18.

  Kibwana Shomari

  Majukumu ya mipira ile ya kurusha ipo kwenye mikono ya nyota huyu mzawa kutoka ilipo milima ya Uluguru, Morogoro.Kibindoni ana pasi moja ya bao kwa msimu wa 2021/22.

  Previous articleNABI:MIMI NI MTU WA KAZI SIO MANENOMANENO
  Next articleMUONEKANO WA UKURASA WA MBELE CHAMPIONI IJUMAA