IMEELEZWA kuwa benchi la ufundi la Namungo FC litafumuliwa hivi karibuni ili kuweza kupata kocha mpya kwenye kikosi hicho.
Habari kutoka ndani ya Klabu ya Namungo zinasema kuwa viongozi wameanza kufanya mazungumzo na aliyekuwa kocha wa Simba na sasa anaifundisha AFC Leopards ya Kenya, Patrick Aussems kuona namna gani watampata.
Inatajwa kuwa Namungo tayari wamemtumia hadi mikataba yao Aussems na wamefanya mazungumzo kwa ukaribu na kocha huyo, kinachosubiriwa ni maamuzi ya pande zote mbili kulingana na hali ilivyo.
Namungo chini ya Kocha Hemed Morocco hadi sasa katika Ligi imeshinda mechi mbili, sare tatu na imepoteza mechi tatu ikiwa na pointi tisa kibindoni.
Mechi ilizoshinda ilikuwa dhidi ya Geita Gold ambao huu ulikuwa ni wa ufunguzi ulichezwa Uwanja wa Ilulu na mchezo wa pili ulikuwa ni dhidi ya Ruvu Shooting.
Kwenye mchezo dhidi ya Ruvu Shooting ungozi wa Namungo ulikuwa unatajwa kuwa mchezo wa kipimo kwao kwa kuwa uongozi uliweza kuwapa mchezo mmoja na kuweka wazi kuwa endapo wangepoteza mchezo benchi la ufundi lingefutwa kazi.
Kwa kuwa walishinda bado benchi hilo lipo ndani ya timu hiyo ambayo ina mastaa wengi ikiwa ni pamoja na Shiza Kichuya, Obrey Chirwa na Jonathan Nahimana.