WACHEZAJI HAWA NI MWENDO WA NGUVU KUBWA UWANJANI

MALENGO yanahitaji nguvu kuyafikia lakini ni lazima na akili pia itumike kwani ikiwa itatumika nguvu nyingi hasara huwa ni kubwa kuliko faida.

Kwa sasa Ligi Kuu Bara baada ya kuanza kuridima tumeanza kushuhudia vitendo vya matumizi ya nguvu nyingi uwanjani jambo ambalo limekuwa likiwafanya wachezaji wengine kushindwa kuendelea na majukumu yao.

Haina maana kwamba nguvu hazipaswi kutumika ila ni pale ambapo inahitajika kwani mlinzi wa mchezaji mwingine ni mchezaji mwenyewe kwa wachezaji nyie mkiwa uwanjani tembezeni amani, upendo na pasi masuala ya vita ya kuumizana wekeni kando hilo haliwahusu.

Mchezaji wa zamani wa timu ya Tanzania na Yanga, Mohamed Hussein, ‘Mmachinga’ amesema kuwa majeraha ni moja ya sababu inayorudisha nyuma maendeleo ya wachezaji hivyo ni lazima kila mmoja awe mlinzi wa mwingine.

Hapa ni baadhi ya wachezaji ambao walionekana wakitumia nguvu nyingi kwenye mechi zao na kuwasababishia maumivu wachezaji wengine namna hii:-

Lwanga

Septemba 25 kwenye mchezo wa ufunguzi wa Ligi Kuu Bara hapa ulishuhudiwa mchezo wa Ngao ya Jamii kati ya Simba v Yanga .

Taddeo Lwanga wakati timu yake ikiwa impeoteza kwa kufungwa bao 1-0 alimchezea faulo Feisal Salum na alionekana akimpiga kiwiko. Alionyeshwa kadi ya njano kwa kuwa alikuwa na kadi mbili za njano alionyeshwa kadi nyekundu na kutolewa nje.

Kutokana na adhabu hiyo alikosa mchezo mmoja wa ligi ilikuwa dhidi ya Biashara United, Uwanja wa Karume, Mara na ubao ulisoma Biashara United 0-0 Simba.

Bangala v Kanoute

Ilikuwa ni kwenye Kariakoo Dabi, Septemba 25, Yanick Bangala alionekana akimchezea faulo kiungo Sadio Kanote na faulo hiyo ilimfanya mwamuzi amuonyeshe Bangala kadi ya njano.

Kutokana na maumivu ambayo aliyapata Kanote aliweza kukosa mechi mbili za ligi ilikuwa ile ya Biashara United pamoja na mchezo dhidi ya Dodoma Jiji, kwa sasa taarifa kutoka Simba zinaeleza kuwa nyota huyo ameanza mazoezi.

Keneddy Juma

Ilikuwa ni Oktoba Mosi, Uwanja wa Jamhuri Dodoma wakati ubao ukisoma Dodoma Jiji 0-1 Simba. Beki wa Simba Keneddy Juma alionekana akipigwa kiwiko na nyota wa Dodoma Jiji Anuary Jabir.

Kutokana na tukio hilo Jabir alionyeshwa kadi nyekundu na kuwa mchezaji wa kwanza msimu wa 2021/22 kuonyeshwa kadi nyekundu ya moja kwa moja.

Oktoba  2, Yanga 1-0 Geita Gold

Ngoma ilikuwa nzito kwa wachimba dhahabu kutoka Mwanza ambapo walipoteza mchezo wao wa pili baada ya ule wa awali kufungwa mabao 2-0 dhidi ya Namungo FC.

Alikuwa ni Amos Kadikilo alionekana akimchezea faulo nyota wa Yanga, Jesus Moloko kwa kumpiga kiwiko ila mwamuzi hakuweza kuona tukio hilo.

Pia nyota mwingine Yusuph Kagoma wa Geita Gold alionekana akimgonga kiungo Feisal Salum ambapo kwa maumivu Fei alishindwa kupokea mkono wa Kagoma.

Septemba 28, Uwanja wa Karume, Mara

Nyota wa Biashara United Mpapi Nasibu alimchezea faulo kiungo wa Simba, Hassan Dilunga na hilo lilisababisha Mpapi kuonyeshwa kadi ya njano.

Kennedy

Kennedy Juma alimchezea faulo Christian Nziga na alionekana akimpiga buti mgongoni ilikuwa ni kwenye mchezo wa ligi na alionyeshwa kadi ya njano.