>

KIUNGO SIMBA AKUBALI KUSAINI YANGA

NICHOLAS Gyan kiungo wa zamani wa Klabu ya Simba ambaye kwa sasa anakipiga ndani ya kikosi cha DTB kinachoshiriki Championship amesema kuwa hana tatizo ikiwa Yanga watampa ofa yeye atasaini kwa kuwa mpira ni kazi yake.

Novemba 29 Gyan aliweza kufunga bao lake la kwanza akiwa na timu yake ya DTB kwenye mchezo dhidi ya Ndanda ambapo walishinda kwa mabao 2-1 jambo ambalo limemuongezea hali ya kujiamini baada ya kurudi Tanzania.

Gyan amesema kuwa anaitambua ligi ya Tanzania kwa uzuri na kwa namna ambavyo alivyo na uzoefu ana imani kwamba timu yoyote ile anaweza kucheza kwa kiwango kikubwa.

“Ninaweza kusema kwamba ikitokea kwa sasa nikapata ofa iwe kutoka Yanga ama timu nyingine yoyote sitaona shida kusaini kama taratibu zitafuatwa kwa kuwa kazi yangu ni mpira.

“Hapa Tanzania ligi yake naijua na namna ushindani ulivyo ninatambua bado sijaona kama ninaweza kushindwa kucheza kwenye ligi kwani hapa nilipo ushindani wake ni mkubwa pia,” alisema Gyan.

Dirisha dogo la usajili linatarajiwa kufunguliwa Desemba 15 mwaka huu.