MSANII wa muziki wa kizazi kipya Bongo, Boniventure Kabogo (Stamina), ameachia album yake ya pili aliyoipa jina la Paradiso ambayo ina mkusanyiko wa jumla ya nyimbo 13.
Wasanii alioshirikiana nao katika albamu hiyo ambayo imezinduliwa kupitia jukwaa la Boomplay, ni pamoja na Bele 9, Aslay, Linah, Walter Chilambo, Saraphina, Isha Mashauzi, Barakah The Prince na wengine kibao.
Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Stamina amewashukuru wote walioshiriki katika maandalizi ya albamu yake kwa kuandika: “Shukrani zangu za dhati ziende kwa wasanii wote ambao nimeshirikiana nao kwenye hii album, producers wote, directors wote na wadau wote tuliopambana kukamilisha albamu hii.”
Stamina ameitaja albumu hiyo kuwa ni albamu bora kwani ameifanya kwa ubunifu na uwekezaji mkubwa, ikiwa ni ya pili tangu aanze muziki baada ya ile ya kwanza aliyoipa jina la ‘Mlima Uluguru’ ambayo ilitoka 2015.
Maprodyuza walioiandaa albamu hiyo ni pamoja na Bear, Sampamba, Papa, Shaska na Walter Chilambo ambapo kupitia albamu hiyo, Stamina anaingia kwenye orodha ya wasanii wa Hip-hop walioachia albamu mwaka huu kupitia Boomplay wakiwemo Dogo Janja ambaye aliachia ‘Asante Mama’ na Rapcha aliyeachia ‘Wanangu 99’.
Unaweza kuisikiliza albamu nzima hapa kwa kubofya: https://www.boomplay.com/share/album/35613974