>

MZEE WA KUCHETUA ATUMA UJUMBE KWA WAZAMBIA

BERNARD Morrison, mzee wa kuchetua ametuma ujumbe kwa Red Arrows ya Zambia kwa kuweka wazi kwamba wanahitaji ushindi kwenye mchezo wao wa marudio katika Kombe la Shirikisho.

Morrison alikuwa ni nyota wa mchezo ule wa kwanza walipokutana Uwanja wa Mkapa licha ya kuwa na changamoto ya maji kwenye ule uwanja aliweza kuhusika kwenye mabao yote matatu.

Alifunga mabao mawili alitoa pasi moja ya bao kwa Meddie Kagere huku akiweka rekodi ya kukosa penalti kwenye mchezo huo uliokuwa na ushindani mkubwa.

Leo Desemba 3, kikosi cha Simba kinatarajiwa kuibukia nchini Zambia na kwenye msafara huo nyota Morrison yupo kwenye kikosi na anatarajiwa kuanza kikosi cha kwanza ikiwa fitina za wapinzani wao zitagonga mwamba.

Morrison amesema:”ushindi wetu kwenye mchezo wa kwanza haukuwa wangu bali ni timu kwa ujumla na hiyo inatufanya tuongeze juhudi kwenye mchezo wetu wa marudio.

“Ushindani ni mkubwa hilo lipo wazi nasi pia tupo tayari kwa ajili ya ushindani mashabiki wawe pamoja nasi bega kwa bega kwa dua na wale ambao watakuja uwanjani ni furaha kwetu,” amesema.

Desemba 5 mchezo wa marudio unatarajiwa kuchezwa ambapo mshindi wa jumla atapata nafasi ya kutinga hatua ya makundi Kombe la Shirikisho na yule ambaye atafungashiwa virago vyake atapaswa kusubiri wakati mwingine akipata nafasi.