Home Sports SIMBA WAMESHINDA ILA CHA MOTO WAMEKIONA

SIMBA WAMESHINDA ILA CHA MOTO WAMEKIONA

MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu Bara Simba leo wameibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Geita Godld baada ya dakika 90 kukamilika lakini cha moto wamekiona.

Mchezo wa leo haukuwa mwepesi kwa Simba wala Geita Gold kwa kuwa timu zote mbili zilikuwa zinaupiga ule mpira wa darasani huku Geita Gold wakicheza kwa kujiamini wakati Simba wakicheza kwa presha kubwa ya kusaka ushindi.

Pablo Franco, Kocha Mkuu wa Simba alikuwa wa kwanza kuona wachezaji wake wakijaza kimiani bao la kuongoza ilikuwa dakika ya 9 kupitia kwa Peter Banda lakini alikuwa anakumbuka kwamba bao la George Mpole dakika ya sita lilikuwa ni la kuotea na mwamuzi alilifuta.

Ngoma ilikwenda mpaka mapumziko ikiwa Simba wanaongoza kwa bao 1-0 lakini mabeki wa Simba hawakuwa makini wakiongozwa na Joash Onyango pamoja na Gadiel Michael akisaidiana na Shomari Kapombe na Kened Juma kwa kuwa wana Geita Gold walikuwa ni moto muda wote wakimtumia Juma Mahadhi.

Mambo yalipokuwa magumu Pablo aliamua kufanya mabadiliko kwa kumtoa kiungo Ibrahim Ajibu ambaye alikosa utulivu leo pamoja na Rally Bwalya na kuingia kwa Bernard Morrison na Mzamiru Yassin ambao hawa angalau walileta uhai kwa Simba upande wa kiungo.

Lilipachikwa bao la pili dakika ya 56 kupitia kwa Mzamiru Yassin na kuwafanya Simba wajiamini kwamba mchezo umemalizika kumbe Geita Gold bado walikuwa wamo.

Bao la Geita Gold lilifungwa na Juma Mahadhi kwa shuti kali lililomshinda Manula na lilifungwa bao lingine kali la pili kwa Geita Gold ila mwamuzi aliligomea ile kwa kile kilichodaiwa kwamba ni mfungaji kuotea.

Ushindi huo unaifanya Simba kufikisha pointi 17 wakiwa nafasi ya pili na Geita Gold inabaki na pointi tano ikiwa nafasi ya 15 kwenye msimamo, vinara ni Yanga wenye pointi 19.

Previous articleDAKIKA 45, SIMBA YAENDA MAPUMZIKO KIFUA MBELE
Next articleNABI ANASA FAILI LA PABLO FRANCO