KUELEKEA kwenye mchezo wa leo wa Simba v Geita Gold, mchambuzi wa masuala ya michezo ndani ya ardhi ya Tanzania, Mussa Mateja ameweka wazi kwamba mchezo wa leo utakuwa na ushindani kwa timu zote mbili.
Simba inayonolewa na Kocha Mkuu, Franco Pablo leo itawakaribisha Geita Gold kwenye mchezo utakaochezwa Uwanja wa Mkapa.
Mateja ameweka wazi kuwa kwa namna ambavyo anavitazama vikosi vyote viwili anaamini kwamba kutakuwa na mabadiliko kidogo kwa Simba kwa kuwa ina mchezo dhidi ya Red Arrows ambao ni wa marudio jambo ambalo litafanya wachezaji wacheze kwa tahadhari kubwa.
Mchambuzi huyo amesema:”Simba imekuwa ikitumia wachezaji wengi wa ndani kikosi cha kwanza na kwa namna ambavyo ninafahamu hakutakuwa na mabadiliko makubwa sana kwenye mchezo wa leo.
“Kuhusu matokeo itategemea namna ambavyo wachezaji wenyewe wanaweza kuanza inaweza kuwa athari kwao ya kupoteza ama kushinda lakini yote yapo mikononi mwa wachezaji wenyewe.
Kuhusu Kocha Mkuu wa Geita Gold, Felix Minziro, Mateja ameweka wazi kuwa wachezaji wake na uzoefu unaweza kuwa tatizo ikiwa hajafanyia kazi makosa ya mechi iliyopita dhidi ya Yanga, Uwanja wa Mkapa.
“Shida inakuja sehemu moja yupo na kikosi kingine tofauti na wakati ule, kumbuka kwamba alikuwa ndani ya Mbao FC ambayo ilikuwa imeshiriki ligi na ina uzoefu.
“Leo anakuwa na timu mpya ya Geita Gold ambayo ameifundisha na kuipadisha hapo kunakuwa na tofauti kwenye suala la uzoefu.
“Ikumbuke ile mechi yake iliyopita dhidi ya Yanga hakukuwa na wachezaji wenye uzoefu licha ya kwamba wapo wenye uzoefu kiasi chake bado walikwama kupata ushindi.
“Ile hali ya wachezaji kushindwa kuwa na uzoefu inawapa ngumu kwenda na kasi, hivyo kama Minziro bado hajafanyia kazi makosa ya mechi iliyopita basi itakuwa ni ngumu kupata matokeo.
“Ukiangalia kwenye ligi kuna timu ambazo zinakamiwa ni Simba na Yanga hivyo tunaamini kwamba itakuwa ni kazi kubwa kwa timu zote kusaka ushindi,” amesema Mateja.