NYOTA HAWA WATANO WA YANGA KUIKOSA NAMUNGO

VINARA wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga kwa sasa wapo ndani ya Ilulu, Lindi kwa ajili ya maandalizi ya mwisho ya mchezo wao wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Namungo FC.

Mchezo huo unatarajiwa kuchezwa kesho, Novemba 20, Uwanja wa Ilulu na itakuwa ni mara ya kwanza kwa Yanga kukutana na Namungo kwenye uwanja huo katika mchezo wa Ligi Kuu Bara kwa kuwa awali walikuwa wanakutana kwenye Uwanja wa Majaliwa ambao kwa sasa unafanyiwa maboresho.

 

Kikosi cha Yanga kimeondoka na wachezaji 23 kueleka katika mchezo huo, na ni wachezaji watano wa kikosi hicho ambao hawatakuwa sehemu ya kikosi hicho.

Yacuba Sogne, Balama Mapinduzi, Dickson Ambundo, na Ramadhani Kabwili hawa wote wanakosekana kutokana na kuwa majeruhi lakini mchezaji Ditram Nchimbi anakosekana kutokana na mambo ya kifamilia.

 

Wakimalizana na Namungo, Yanga kituo kinachofuata ni Mbeya ambapo Novemba 30 watacheza na Mbeya City, Uwanja wa Sokoine.

Yanga ni timu pekee iliyoshinda michezo yote mitano (5) ya Ligi Kuu wakiwa wanaongoza ligi kwa alama 15 tofauti ya alama nne (4) dhidi ya Simba SC wanoshika nafasi ya pili wakiwa na alama 11.