Home Uncategorized KOCHA YANGA AOMBA KAZI SIMBA … SOMA HAPA

KOCHA YANGA AOMBA KAZI SIMBA … SOMA HAPA

KATIKA rundo la CV ambazo Simba imezipokea kwa ajili ya nafasi ya kocha mkuu wa timu hiyo, kuna majina ya makocha kadhaa waliowahi kuifundisha Yanga.

Simba sasa inasaka mrithi wa Mfaransa, Didier Gomes, aliyetangaza kujiuzulu klabuni hapo baada ya matokeo mabaya kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika.

 

Baadhi ya makocha waliowahi kuifundisha Yanga wanaitajwa zaidi ni Mholanzi, Hans Van Der Pluijm, Mserbia, Zlatko Krmpotić na Mserbia, Kostadin Papic.

 

Tayari uongozi wa Simba umeanza mchakato wa kumsaka kocha mpya baada ya Gomes kusitisha ajira yake kufuatia kuondolewa katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Jwaneng Galaxy ya Botswana.

Simba inasaka kocha mpya lakini ambaye atakuwa na leseni ya Daraja A la Shirikisho la Soka Afrika (Caf) au ile ya
Daraja A ya Shirikisho la Soka Ulaya (UEFA pro) ambayo Gomes hakuwa nayo hali iliyoondoa sifa yake ya kukaa
kwenye benchi katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika inayosimamiwa na Caf.

 

Chanzo chetu kutoka Simba kimesema, hadi sasa kuna CV nyingi za makocha wakiwemo waliofundisha Yanga pia kuna makocha wakubwa Afrika kutoka katika baadhi ya timu ambazo zimetinga hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Timu zilizotinga makundi Ligi ya Mabingwa Afrika ni Al Ahly ambayo kocha wake ni Pitso Mosimane, Espérance
ambayo inanolewa na Radhi Jaidhi, Wydad Casablanca inayonolewa na Walid Regragui, Mamelodi Sundowns
inayonolewa na Rulani Mokwena, Horoya inayonolewa na Lamine N’Diaye, Étoile du Sahel inayonolewa na Lassaad
Dridi, Al Hilal iliyo chini ya kocha Leonardo Jardim, CR Belouizdad ya kocha Beketi Karim, Petro de Luanda ya
kocha José Neto na ES Sétif inayofundishwa na Nabil Kouki.

 

Nyingine ni Al Merrikh ya kocha Lee Clark, Sagrada Esperança chini ya kocha Rui Sapiri, Jwaneng Galaxy inayofundishwa na Miguel da Costa na AmaZulu ya kocha Benni McCarthy.

“Kweli mchakato wa kumpata kocha mpya, umeashaanza na sasa tuna CV nyingi sana mezani kwetu, ila kubwa
tunaendelea kuangalia ni vigezo vipi tutatumia kumpata aliye bora zaidi kwani ni wazi kuwa kila mmoja wetu anafahamu kuwa Simba inahitaji kocha mkubwa mwenye uzoefu na soka la nje na ndani,” kilisema
chanzo hicho.

Championi lilimtafuta mmoja wa wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi Simba, Mulamu Ng’ambi ambaye alisema:
“Ni kweli hadi sasa baada ya ulimwengu kujua kuwa tumeachana na kocha wetu Gomes, kuna maombi mengi
sana yapo ila hatujaanza kupitia CV moja baada ya nyingine.

“Kama ilivyo kawaida ya makocha kila wakisikia suala la nani kaondoka, huwa wanaomba sana kazi hata waliopo kwenye ajira hadi muda huu, kubwa unatakiwa ujue kwamba waliowasilisha CV kwetu hadi sasa wapo makocha wakubwa na wengine tayari wameshafuzu hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

 

“Hivyo utagundua kuwa Simba inahitajika na makocha wengi sana, mbali na hivyo kuna CV hadi za makocha waliowahi kweli kuzinoa Yanga na timu za taifa za hapa Afrika na wengine Ulaya, hivyo bado tunaangalia ni lini tutakaa na kupitia CV moja baada ya nyingine.

“Ninachoweza kukuambia kwa sasa ni kwamba wewe endelea kuvuta subira kwani mara tutakapompata kocha anayehitajika kuinoa Simba tutaliweka wazi hilo, kwani lengo letu ni kuhakikisha tunapata kocha mwenye hadhi ya Simba.”

 

 

 

 

 

Previous articleCITY YAONJA JOTO YA JIWE BAADA YA MIAKA MITANO
Next articleHUKUMU YA MORRISON NA CAS KUTOLEWA