KLABU ya Manchester United inatajwa kuwa mbioni kumfukuza kazi kocha wake, Ole Gunner Solskjaer baada ya kipigo cha 5-0 kutoka Liverpool.
Kichapo hicho kimewakasirisha wengi ikiwa ni pamoja na mashabiki jambo ambalo limewafanya wasiwe na imani na kocha huyo.
Taarifa zimeeleza kuwa mabosi wa United wamewasiliana na Kocha Antonio Conte ili kukaa mezani na kuzungumza uwezekano wa kurithi mikoba ya Solskjaer na Sky Sports Italia imethibitisha.
Conte mwenye miaka 52 ni mzaliwa wa Lecce Italia na amewahi kufundisha timu kubwa kama Chelsea 2016-2018 na Inter Milan 2019-2021.
Haya yanajiri baada ya Man United kuchezea kipigo cha bao 5-0 kutoka kwa mahasimu wao, Liverpool na nyota kutoka Misri, Mohamed Salah alifunga hat trick kwenye mchezo huo.
Man United wamekuwa na mwendelezo wa matokeo yasiyoridhisha kwa siku za hivi karibuni licha ya uwepo wa nyota wao, Cristiano Ronaldo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Klabu ya Manchester, Richard Arnold amevunja appointment zote za vikao vya wageni ili kukutana na Mmiliki wa Klabu hiyo, Joel Glazer kwa ajili ya kujadili hatima ya Kocha wa Klabu hiyo, Ole Gunnar Solskjaer baada ya kipigo cha jana.