>

PACHA YA BANGALA,JOB NA DJUMA YAJIBU YANGA

PACHA ya nyota watatu ambao ni mabeki ndani ya kikosi cha Yanga kinachonolewa na Kocha Mkuu, Nasreddine Nabi imejibu baada ya kuweza kucheza kwenye mechi tatu ambazo ni sawa na dakika 270 bila kuokota mpira nyavuni.

Ndani ya Ligi Kuu Bara, Yanga imecheza mechi tatu ambapo ile ya kwanza ilikuwa mbele ya Kagera Sugar, Uwanja wa Kaitaba na ilishinda kwa bao 1-0 na mchezo wa pili ulichezwa Uwanja wa Mkapa dhidi ya Geita Gold na timu hiyo ilishinda kwa bao 1-0.

Mchezo wa tatu ulipigwa Songea, Uwanja wa Majimaji na ubao ulisoma KMC 0-2 Yanga na kuipa pointi tatu mazima timu hiyo ambayo kwa sasa ina pointi tisa kibindoni.

Nabi amekuwa akiwatumia mabeki wake watatu kulinda mikono ya kipa wake Diarra Djigui ambaye amekaa langoni kwenye mechi hizo zote akiwa salama mbele ya ukuta wa Dikson Job ambaye ni mzawa, Yanick Bangala na Djuma Shaban hawa ni raia wa DR Congo.

Mabeki hao watatu wamekuwa ni wakazi zote chafu ndani ya Yanga kwani Job licha ya kuwa na umbo dogo na mfupi kwa muonekano ni balaa kwa mipira ile ya juu huku Bangala akiwa ni mtibua mipango na mtoa maelekezo kwa wachezaji wengine akishirikiana na Djuma.

Akizungumza na Saleh Jembe, Job alisema kuwa wamekuwa na ushirikiano mkubwa na wachezaji wote jambo ambalo linawafanya waweze kujiamini.

“Kwa upande wa muunganiko ninaona kwamba tunafanya vizuri na kila mchezaji anatimiza jambo lake kwa wakati hivyo ni jambo la furaha kwetu,” alisema.

Pia mabeki hao wanakumbuka kwamba waliweza kucheza mchezo wa Ngao ya Jamii mbele ya Simba na kuibuka na ushindi wa bao 1-0 ilikuwa Uwanja wa Mkapa.

Mchezo ujao wa Yanga ni dhidi ya Azam FC unatarajiwa kuchezwa Uwanja wa Mkapa, Dar itakuwa ni Oktoba 30.