>

NDAYIRAGIJE AFUNGASHIWA VIRAGO GEITA GOLD

ETIENNE Ndayiragije anakuwa kocha wa kwanza kuchimbishwa ndani ya Ligi Kuu Bara msimu wa 2021/22 ambapo alikuwa ni Kocha Mkuu wa Geita Gold.

Taarifa iliyotolewa na Geita Gold imeeleza kuwa ni makubaliano ya pande zote mbili baada ya kocha huyi kushindwa kufikia malengo ambayo yapo kwenye makubaliano.

Kwa sasa timu hiyo ambayo jana Oktoba 23 ililazimisha sare ya kufungana bao 1-1 dhidi ya Mbeya City itakuwa mikononi mwa Fred Felix Minziro ambaye ni kocha msaidizi.

Timu hiyo ambayo inashiriki msimu huu Ligi Kuu Bara haikuanza vizuri katika mchezo wa ufunguzi ambapo ilipoteza kwa kufungwa bao 1-0 dhidi ya Namungo FC, Uwanja wa Ilulu.

Kwenye mchezo wa pili ilipoteza pia kwa kufungwa bao 1-0 dhidi ya Yanga mchezo huu ulichezwa Uwanja wa Mkapa jambo ambalo liliwafanya mabosi wa timu hiyo kuzungumza na kocha huyo kuhusu mwendo wa timu.

Ni mechi nne ambazo amekaa benchi na amekusanya pointi mbili ikiwa nafasi ya 13 kwenye msimamo na vinara ni Yanga wenye pointi tisa baada ya kucheza mechi tatu.