BENCHI la ufundi la Simba limebainisha kuwa kazi bado inaendelea kuelekea kwenye mchezo wao wa marudio dhidi ya Jwaneng Galaxy unaotarajiwa kuchezwa Uwanja wa Mkapa leo.
Katika mchezo wa uliochezwa Uwanja wa taifa wa Botswana, Simba ilishinda kwa mabao 2-0 hivyo ina mtaji wa mabao kibindoni jambo linalowapa hali ya kujiamini kuelekea kwenye mchezo wao wa marudio.
Akizungumza na Saleh Jembe, Kocha Msaidizi wa Simba ambaye alikaa benchi nchini Botswana, Hitimana Thiery amesema kuwa wanafurahi kupata ushindi ugenini lakini lazima wapambane kupata ushindi kwenye mchezo wao wa pili.
“Ushindi wa kwanza ni jambo la furaha kwetu lakini haina maana kwamba kazi imeisha bado tunaendelea na lazima tutumie akili kupambana na wapinzani wetu hasa ukizingatia kwamba tayari wameshajua mbinu zetu na wanatufuatilia pia.
“Kwenye mchezo wa kwanza tulipata tabu kupata video zao za mechi za hivi karibuni lakini tuna amini kwamba uzoefu wa wachezaji pamoja na ile shauku ya kushinda mechi zetu utatupa nguvu na kila kitu kitakuwa sawa,” amesema Hitimana.