NASREDDINE Nabi, Kocha Mkuu wa Yanga alitambulishwa ndani ya kikosi hicho ilikuwa ni Aprili 20 na alianza kazi yake ya kwanza katika mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Azam FC uliochezwa Uwanja wa Mkapa.
Katika mchezo huo uliochezwa Aprili 24, Nabi alishuhudia Uwanja wa Mkapa ubao ukisoma Azam FC 1-0 Yanga hiyo ilikuwa inaitwa karibu Dar na alianza na kichapo kwenye maisha yake ya soka Bongo.
Ni miezi sita tayari imeshameguka kwa kocha huyo kuwa ndani ya Yanga ambayo inapointi tisa kwa sasa ndani ya Ligi Kuu Bara ikiwa imeshinda mechi zote tatu ambazo ilicheza kwenye ligi na kufunga jumla ya mabao manne kibindoni.
Jumla amekaa kwenye benchi katika mechi 24 ambapo ni kwenye mashindano yote kuanzia Ligi Kuu Bara, Ngao ya Jamii, ya kirafiki, Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho.
Katika michuano ya Kagame Cup iliyofanyika Julai mwaka huu hapa Tanzania hakuweza kuwa kwenye benchi la ufundi kwa sababu alikuwa likizo.
Katika mechi 24 ambazo amesimamia alishinda mechi 17, sare mbili na aliambulia kichapo kwenye mechi zake tano huku safu yake ya ushambuliaji ikifunga jumla ya mabao 30.
Ule ukuta wa safu ya ulinzi umeruhusu mabao ya kufungwa 13 na kwenye mechi 14 aliweza kushuhudia vijana wake wakitoka wababe bila kuokota mpira kwenye nyavu zake.
Nabi msimu wa 2021/22 ameuanza kwa mguu wa kulia baada ya timu yake kusepa na taji la Ngao ya Jamii baada ya kushinda bao 1-0 mbele ya Simba kwenye mchezo uliochezwa Uwanja wa Mkapa.
Ni bao la Fiston Mayele dakika ya 11 ambalo liliwafanya waweze kusepa na taji hilo ambalo wanatamba nalo kwa sasa kitaa huku mashabiki wakiwa na imani ya kuweza kutwaa pia taji la Ligi Kuu Bara ambalo lipo mikononi mwa Simba.
Leo Oktoba 24 anatimiza jumla ya siku 187 baada ya kutambulishwa kuwa Kocha Mkuu wa Yanga na lugha ambayo anaongea ni kiarabu pia ana uwezo wa kuzungumza Kiingereza ikiwa ataamua kufanya hivyo.
Kwa msimu wa 2020/21 mfungaji bora kwenye kikosi chake alikuwa ni Yacouba Songne ambaye alifunga mabao nane ndani ya Ligi Kuu England.