MBELE ya mashabiki 72,279 Manchester United walipindua meza kibabe na kusepa na pointi tatu mazima katika mchezo ambao ulionekana kuwa mgumu kwao dakika 45 za mwanzo ila baada ya dakika 90 ubao ukasoma Manchester United 3-2 Atalanta katika mchezo wa UEFA Champions League na unawafanya wawe namba moja katika kundi F baada ya kufikisha pointi 6.
Uwanja wa Old Trafford uliokusanya jumla ya mabao matano ni mawili ya Atalanta ambao walitangulia kuwatungua United ilikuwa dakika ya 15 kupitia kwa Mario Pasalic na Merih Demiral dakika ya 28 na kuwafanya United kwenda mapumziko wakiwa nyuma kwa mabao mawili.
Ngoma ilipinduliwa kipindi cha pili na vijana wa Ole Gunnar Solskjaer Kocha Mkuu wa United ambaye alishuhudia mabao yakipachikwa na Marcus Rashford dakika ya 53,Harry Maguire dakika ya 75 huku msumari wa mwisho na wa ushindi ukipachikwa na Cristiano Ronaldo dakika ya 81 ambaye aliwaka kwa furaha baada ya kuipa pointi tatu timu yake.
Katika mchezo huo nyota Marcus Rashford aliweza kuanza kikosi cha kwanza tangu alipofanya hivyo Mei katika fainali ya Europa ambapo alichukua nafasi ya Jadon Sancho huku Bruno Fernandes akichaguliwa kuwa nyota wa mchezo.