ISHU YA UWANJA YAMSHANGAZA KOCHA,KESHO STARS KAZINI

KOCHA wa Timu ya Taifa ya Tanzania Taifa Stars Kim Poulsen amesikitishwa na kitendo cha Mamlaka za soka kuinyima ruhusa timu hiyo ya Taifa kupata nafasi ya kufanya mazoezi kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.

 Poulsen amebainisha kuwa anajisikia vibaya na anshindwa kuelewa dhana ya kuinyima timu ya taifa faida ya kufanya mazoezi na maandalizi ya mechi kwenye nyasi halisi za Uwanja wa Mkapa na badala yake wanapelekwa kwenye nyasi za bandia ilihali mchezo dhidi ya Somalia utachezwa katika Uwanja wa Benjamini Mkapa.

Amesisitiza kuwa kitendo cha Taifa Stars kunyimwa fursa angalau siku moja kabla ya mechi hiyo huku mashindano ya U-20 yakipewa kipaumbele kuliko Taifa Stars ni jambo linaloshangaza.

“Nashangaa na kiukweli nashindwa kuelewa, kwamba tunapokuwa Taifa Stars tunacheza mchezo wa kufuzu Fainali za CHAN,mchezo muhimu na haturuhusiwi kufanya mazoezi kwenye Uwanja wa Taifa!

Aidha Poulsen amebainisha kuwa wachezaji wote wapo kwenye hali nzuri isipokuwa beki wa kushoto David Luhende ambaye anasumbuliwa na maumivu ya misuli ambaye amethibitisha kuwa hatahusika kabisa kwenye mchezo huo wa kesho.

Taifa Stars inatarajiwa kucheza michezo miwili ya mtoano dhidi ya Somalia ambapo atakayeibuka mshindi atacheza dhidi ya Uganda ili kupata mshindi atakayefuzu kushiriki fainali za CHAN.