MZUNGUKO WA PILI UNAANZA,WAZEE WA MIGODI LEO KAZINI

MZUNGUKO wa pili ndani ya Ligi Kuu Tanzania Bara, leo Februari 25 unatarajiwa kuanza kwa ajili ya timu kusaka pointi tatu muhimu.

Ni matajiri wa dhahabu, Geita Gold watamenyana na matajiri kutoka mgodini huko Lindi, Namungo FC.

Geita Gold wameweka wazi kwamba Uwanja wa Nyankumbu upo tayari kufanya kile ambacho wamekizoea wakiwa kwenye uwanja wao bora.

Ikumbukwe kwamba walipokutana kwenye mchezo wa mzunguko wa kwanza, Uwanja wa Ilulu, Lindi ubao ulisoma Namungo 2-0 Geita Gold na ilikuwa ni Septemba 27,2021.

Mpambayange Abdalah, Mratibu wa Geita Gold amesema kuwa wapo tayari kwa ajili ya mechi zote za mzunguko wa pili na wanahitaji kupata pointi tatu muhimu.

“Tupo tayari kwa ajili ya mechi zetu zijazo na tukiwa Uwanja wa Nyakumbu tunapata matokeo mazuri hili ni jambo zuri kwetu, mashabiki wazidi kuwa pamoja nasi,”.

Kwenye msimamo Geita Gold ipo nafasi ya 6 ikiwa na pointi 20 na Namungo FC ipo nafasi ya 4 ikiwa na pointi 23.