Ronaldo Aondoka Kambini Portugal Baada ya Kocha Kukataa Madai ya Mgogoro

Cristiano Ronaldo ameondoka kwenye kambi ya timu ya taifa ya Portugal na kusema atakuja kueleza sababu za uamuzi huo “kwa wakati muafaka.”

Uamuzi huo umefanyika muda mfupi baada ya kocha wa Portugal, Jorge Jesus, kukataa taarifa za kuwepo kwa mgogoro kati yake na nahodha huyo mwenye umri wa miaka 41.

Ronaldo aliitwa kwenye kikosi cha wachezaji 25 kwa ajili ya mechi za kimataifa za kipindi hiki na alianza mchezo dhidi ya Wales. Hata hivyo, hakushiriki katika ushindi wa Portugal wa mabao 2-1 dhidi ya Norway mjini Oslo Jumapili.

Baada ya mchezo huo, Ronaldo hakwenda kuwashukuru mashabiki pamoja na wachezaji wenzake, bali alielekea moja kwa moja vyumba vya kubadilishia nguo. Hali hiyo ilizua taarifa kwamba huenda hakuwa ameridhishwa na uamuzi wa kocha.

Akizungumza kabla ya mchezo wa Portugal dhidi ya Denmark, Jesus alisema hakukuwa na tukio lolote la mgogoro.

Kocha huyo alisema alimweleza Ronaldo kabla ya mchezo dhidi ya Norway kwamba hataanza mchezo, lakini angeweza kumuingiza baadaye. Hata hivyo, Jesus aliamua kutomuingiza kabisa.

Jesus pia alikanusha taarifa kwamba Ronaldo alikataa kufanya mazoezi Jumanne, akisema mshambuliaji huyo alipewa mazoezi binafsi ya mobility na strengthening, kabla ya kutarajiwa kufanya mazoezi ya kawaida pamoja na wenzake.

Hata hivyo, Ronaldo hakuonekana uwanjani pamoja na kikosi nchini Denmark, na baadaye alitangaza kupitia Instagram kwamba ameondoka kwenye kambi ya timu ya taifa.

Ronaldo aliandika kwamba baada ya mkutano na vyombo vya habari wa timu ya taifa na mazungumzo na rais wa Shirikisho la Soka la Portugal, aliamua kuondoka kambini.

Amesema “kwa wakati muafaka” atawaeleza Wareno ukweli kuhusu sababu zilizomfanya achukue uamuzi huo.

Shirikisho la Soka la Portugal limethibitisha kuondoka kwa Ronaldo na kusema maandalizi ya timu kwa mechi zinazofuata yataendelea kama ilivyopangwa, huku wachezaji 24 waliosalia wakiendelea na programu ya timu.

Ronaldo, ambaye kwa sasa anacheza katika klabu ya Al-Nassr, alikuwa ametajwa kuwa anaendelea kucheza soka la kimataifa huku akilenga kufikisha mabao 1,000 katika maisha yake ya soka.