Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini Nigeria (NFF) limemtangaza na kumtambulisha rasmi Nabil Nafhezi kuwa kocha mkuu mpya wa timu ya taifa ya wanaume ya nchi hiyo, maarufu kama Super Eagles.
Utambulisho huo unahitimisha wiki kadhaa za sintofahamu kuhusu kocha ambaye angekabidhiwa jukumu la kuiongoza timu hiyo yenye maskani yake jijini Abuja.
Nafhezi anarithi mikoba ya kocha wa zamani, José Peseiro, raia wa Ureno, ambaye aliondoka katika kikosi hicho baada ya mkataba wake kumalizika.
Peseiro alimaliza kipindi chake akiwa ameifikisha Super Eagles hadi hatua ya nusu fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON), ambako timu hiyo ilipoteza dhidi ya wenyeji wa michuano hiyo.
Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika katika makao makuu ya NFF, uongozi wa shirikisho hilo umeeleza kuwa Nafhezi amechaguliwa kutokana na uzoefu na wasifu wake, pamoja na uwezo wake wa kukuza na kuendeleza vipaji vya wachezaji vijana.
Jukumu lake la kwanza litakuwa kurekebisha mwenendo wa Super Eagles katika kampeni za kufuzu Kombe la Dunia, sambamba na kuandaa kikosi kwa ajili ya michuano ijayo ya Kombe la Mataifa ya Afrika.
Akizungumza mara baada ya kukabidhiwa jezi ya timu hiyo, Nafhezi amesema anatambua ukubwa wa jukumu alilokabidhiwa pamoja na matarajio makubwa ya mashabiki wa Nigeria.
Ameahidi kujenga timu itakayocheza soka la kushambulia, lenye nidhamu na ushindani, huku akiomba ushirikiano na sapoti kutoka kwa wadau wote wa soka nchini Nigeria ili kufikia malengo yaliyowekwa.
Mabadiliko hayo ya benchi la ufundi yanatajwa na wachambuzi wa soka barani Afrika kuwa yanaweza kuwa mwanzo wa sura mpya kwa Super Eagles, timu inayojivunia kuwa na wachezaji wengi wanaocheza soka la kulipwa katika ligi mbalimbali barani Ulaya.