DAR ES SALAAM: Klabu ya Azam FC imetangaza kwa masikitiko makubwa kifo cha kipa wa timu yake ya vijana chini ya miaka 20 (U-20), Iddy Salim, aliyefariki dunia kwa ghafla baada ya kupata ajali ya pikipiki (bodaboda) Alhamisi.
Kwa mujibu wa taarifa ya klabu hiyo, mwili wa marehemu ulipelekwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mwananyamala (MRRH), jijini Dar es Salaam, kwa ajili ya taratibu za mwisho kabla ya kusafirishwa kwenda Tanga, nyumbani kwao, kwa ajili ya mazishi.
Uongozi wa Azam FC umetuma salamu za rambirambi kwa familia ya marehemu, ndugu, jamaa na marafiki, pamoja na wote walioguswa na msiba huo, huku ukiwaombea nguvu, faraja na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu.
Kifo cha Iddy Salim kimeacha simanzi kubwa ndani ya klabu hiyo, hasa kutokana na mchango wa Azam FC katika kukuza vipaji kupitia mfumo wake wa vijana.

Marehemu alikuwa miongoni mwa vijana waliokuwa wakijenga taaluma yao ya soka ndani ya klabu hiyo, huku safari yake ikiwa bado changa na ikiwa na matumaini makubwa ya kufikia hatua za juu zaidi katika soka.
Azam FC, iliyoanzishwa mwaka 2004 na inayomilikiwa na Kundi la Bakhresa, imeendelea kujijenga kama moja ya klabu zinazowekeza kwa kiasi kikubwa katika maendeleo ya soka nchini, hususan katika miundombinu na uendelezaji wa vipaji vya vijana.
Inna Lillahi wa Inna Ilayhi Raji’un.
