Mshambuliaji wa Tanzania, Clara Luvanga, amejiunga rasmi na klabu ya Washington Spirit ya Marekani akitokea Al-Nassr ya Saudi Arabia, katika hatua inayomfungulia ukurasa mpya wa safari yake ya soka.
Luvanga, ambaye amekuwa miongoni mwa wachezaji muhimu katika soka la wanawake Tanzania, ameweka historia kwa kuwa Mtanzania wa kwanza kucheza katika Ligi ya Taifa ya Soka la Wanawake Marekani, National Women’s Soccer League (NWSL).
Ripoti zinaeleza kuwa Washington Spirit imelipa takribani dola milioni 2.3 kwa ajili ya kumsajili Luvanga. Endapo kiasi hicho kitathibitishwa rasmi, uhamisho huo utakuwa miongoni mwa uhamisho wenye thamani kubwa katika historia ya soka la wanawake.
Luvanga amekuwa na kipindi bora akiwa Al-Nassr, ambapo msimu wa 2025/26 alifunga mabao 24 na kutwaa tuzo ya mfungaji bora wa ligi.
Kuhamia Marekani kunamfungulia Luvanga fursa mpya ya kuendelea kuonyesha uwezo wake katika moja ya ligi zinazokua kwa kasi katika soka la wanawake duniani.
Uhamisho huo pia unaongeza mwonekano wa vipaji kutoka Tanzania katika soka la kimataifa, huku mafanikio yake yakitarajiwa kuwa chachu ya kufungua fursa zaidi kwa wachezaji wa Tanzania wanaolenga kucheza katika ligi kubwa nje ya nchi.