UEFA Yatingisha Kengele FIFA Baada ya Mpango wa Infantino Kuhusu Kombe la Dunia

Mvutano mkubwa umeanza kushika kasi katika ulimwengu wa soka baada ya kuibuka kwa taarifa kwamba Rais wa FIFA, Gianni Infantino, anafikiria kuleta mfumo mpya wa kibiashara utakaowaruhusu wawekezaji binafsi kumiliki sehemu ya thamani ya Kombe la Dunia.

Kwa mujibu wa taarifa hizo, FIFA inapanga kuanzisha kampuni maalum ambayo itakuwa na nafasi ya kupokea uwekezaji kutoka kwa makampuni binafsi yatakayoweza kununua hisa ndani yake. Mpango huo umeibua mjadala mkali miongoni mwa wadau wa soka, hasa barani Ulaya.

Shirikisho la Soka la Ulaya (UEFA) limeonyesha kutoridhishwa na hatua hiyo na linatarajiwa kufanya kikao maalum kujadili athari zinazoweza kujitokeza endapo mpango huo utaendelea.

Baadhi ya taarifa zimeeleza kuwa huenda mataifa ya Ulaya yakafikiria hatua kali zaidi ikiwemo kutishia kususia michuano ya Kombe la Dunia, ikiwa kutakuwa na mabadiliko makubwa katika namna mashindano hayo yanavyoendeshwa.

UEFA kupitia taarifa yake imeikosoa hatua hiyo, ikisema pendekezo hilo limevuka mipaka ya uendeshaji wa kawaida wa soka na kutaka uwazi zaidi kuhusu manufaa ya kifedha yatakayopatikana.

“Roho na uongozi wa soka si mali za kuuzwa, hasa bila uwazi kuhusu nani atanufaika kifedha,” ilisema UEFA katika sehemu ya taarifa yake.

Hatua hiyo imeongeza mvutano kati ya FIFA na UEFA, huku wadau wa soka duniani wakisubiri kuona kama mpango huo utaendelea au utazua mabadiliko makubwa katika mfumo wa uendeshaji wa michuano mikubwa zaidi ya soka duniani.