Klabu ya Chelsea imekamilisha usajili wa kiungo mshambuliaji wa kimataifa wa England, Morgan Rogers, kutoka Aston Villa kwa mkataba wa hadi mwaka 2033.
Kwa mujibu wa taarifa za vyombo vya habari nchini England, Chelsea imelipa kiasi cha takribani pauni milioni 117 (zaidi ya Shilingi bilioni 400 za Tanzania), jambo lililomfanya Rogers kuwa mchezaji ghali zaidi kutoka Uingereza katika historia ya soka.
Ada hiyo imevuka rekodi ya awali iliyokuwa ikishikiliwa na kiungo Elliot Anderson aliyesajiliwa na Manchester City kutoka Nottingham Forest kwa ada iliyofikia pauni milioni 116.
Chelsea awali ilikuwa na rekodi ya usajili wa bei kubwa kupitia kiungo wa Ecuador, Moisés Caicedo, aliyenunuliwa kutoka Brighton & Hove Albion kwa pauni milioni 115 mwaka 2023.
Rogers mwenye umri wa miaka 22 ameondoka Aston Villa baada ya kuitumikia kwa misimu miwili, ambapo alikuwa sehemu ya kikosi kilichotwaa taji la Europa League mwezi Mei baada ya kuifunga Freiburg mabao 3-0 katika fainali.
Akizungumza baada ya kusaini mkataba huo, Rogers alisema amefurahia kujiunga na Chelsea akieleza kuwa ni klabu kubwa ambayo amekuwa akiipenda tangu akiwa mtoto.
“Chelsea ni klabu kubwa zaidi London na nimekuwa nikiivutiwa nayo tangu utotoni. Ninafurahia mradi wa kocha mpya, wachezaji waliopo na mwelekeo ambao klabu inaenda,” alisema Rogers.
Rogers ana uwezo wa kucheza nafasi ya winga pamoja na kiungo mshambuliaji, na anatarajiwa kuwa sehemu muhimu ya mipango ya Chelsea katika msimu mpya wa Ligi Kuu England.