Brazil imefuzu hatua ya 16 bora ya Kombe la Dunia 2026 baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Japan katika mchezo wa hatua ya 32 bora uliochezwa kwenye Uwanja wa NRG, Houston, Marekani.
Shujaa wa Brazil alikuwa mshambuliaji wa Arsenal, Gabriel Martinelli, aliyefunga bao la ushindi katika dakika ya tano ya muda wa nyongeza, akimalizia mchezo uliokuwa na ushindani mkubwa.
Japan ndiyo iliyokuwa ya kwanza kupata bao kupitia Kaishu Sano katika dakika ya 29 baada ya shambulizi la kushtukiza lililoiacha safu ya ulinzi ya Brazil ikiwa imeshindwa kujipanga.
Brazil ilionekana kuyumba baada ya bao hilo huku Japan ikidhibiti mchezo vizuri hadi mapumziko.
Kocha Carlo Ancelotti alifanya mabadiliko muhimu mwanzoni mwa kipindi cha pili kwa kumwingiza mshambuliaji Endrick badala ya kiungo Lucas Paqueta, hatua iliyoongeza nguvu katika safu ya ushambuliaji ya Brazil.
Mabadiliko hayo yalizaa matunda dakika ya 56, Casemiro akifunga bao la kusawazisha kwa kichwa baada ya kupokea krosi nzuri iliyopigwa na Gabriel Magalhaes.
Japan ilionekana kuwa njiani kupeleka mchezo katika dakika za nyongeza, lakini ilifanya kosa la kupoteza mpira karibu na eneo lake la hatari katika muda wa nyongeza. Brazil ilitumia nafasi hiyo haraka, mpira ukamfikia Gabriel Martinelli ambaye alitulia kabla ya kuupiga wavuni na kuipa timu yake ushindi wa mabao 2-1.
Kwa ushindi huo, Brazil imefuzu hatua ya 16 bora ambapo itakutana na mshindi wa mchezo kati ya Ivory Coast na Norway, huku ikiendelea kuonyesha dhamira ya kupigania ubingwa wa Kombe la Dunia 2026.