Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) imewaondoa kwenye orodha ya waamuzi kwa mizunguko mitano mwamuzi wa kati Hance Mabena kutoka Tanga pamoja na mwamuzi msaidizi namba moja Frank Komba kutokana na mapungufu ya kiuchezeshaji yaliyojitokeza katika mchezo kati ya Simba SC na Pamba Jiji FC.
Adhabu hiyo imetangazwa Juni 18, 2026 baada ya kamati kubaini kuwa waamuzi hao walishindwa kutafsiri kwa usahihi sheria za mchezo wa mpira wa miguu katika mechi hiyo iliyochezwa kwenye Uwanja wa KMC Complex, ambapo Simba iliibuka na ushindi wa bao 1-0.
Mbali na adhabu hiyo kwa waamuzi, Simba SC imetozwa faini ya Shilingi milioni 10 kutokana na kitendo cha mashabiki wake kumwagia maji mwamuzi msaidizi Frank Komba wakipinga uamuzi wake wa kuashiria kuotea (offside) kwa mchezaji wa Simba.
Kwa mujibu wa TPLB, tukio hilo ni kosa la kujirudia kwa mashabiki wa Simba, kwani ndani ya msimu wa 2025/2026 wamehusishwa na matukio mengine matatu yenye mfanano wa ukiukwaji huo, yaliyosababisha klabu hiyo kuadhibiwa mara kadhaa.
Wakati huohuo, Pamba Jiji FC nayo imetozwa faini ya Shilingi laki tano baada ya wachezaji wake sita kuonyeshwa kadi za njano katika mchezo huo.
Hatua hizo zinaonyesha msimamo wa TPLB katika kuhakikisha sheria, nidhamu na viwango vya uchezeshaji vinafuatwa katika mechi za NBC Premier League.