Nahodha wa Ufaransa, Kylian Mbappe, amefunga mabao mawili na kuiongoza timu yake kuibuka na ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Senegal katika mchezo wa Kundi I wa Kombe la Dunia uliochezwa mjini East Rutherford, Marekani.
Nyota huyo wa Real Madrid aliendelea kuandika historia baada ya kufikisha mabao 14 katika Kombe la Dunia, akibakiwa na mabao mawili pekee kufikia rekodi ya mfungaji bora wa muda wote wa michuano hiyo, Miroslav Klose mwenye mabao 16.
Baada ya kipindi cha kwanza kumalizika bila mabao huku Senegal wakionekana kuwa bora zaidi, Ufaransa walibadilika kipindi cha pili na kupata bao la kwanza dakika ya 66 kupitia Mbappe aliyemalizia pasi safi kutoka kwa Michael Olize.
Mshambuliaji wa Paris Saint-Germain, Bradley Barcola, aliyeingia akitokea benchi aliongeza bao la pili dakika za mwisho kabla ya Ibrahim Mbaye kuifungia Senegal bao la kufutia machozi katika muda wa nyongeza.
Hata hivyo, Mbappe alihakikisha ushindi wa Ufaransa kwa kufunga bao la tatu dakika ya 96 kwa shuti kali la mbali, bao ambalo pia lilimfanya kuwa mfungaji bora wa muda wote wa timu ya taifa ya Ufaransa akiwa na mabao 58.
Ushindi huo unaipa Ufaransa mwanzo mzuri wa kampeni yao ya kusaka taji la tatu la Kombe la Dunia chini ya kocha Didier Deschamps, ambaye amethibitisha kuwa mashindano haya yatakuwa ya mwisho kwake kuinoa timu hiyo baada ya miaka 14 madarakani.
Licha ya kushindwa, Senegal walionesha ushindani mkubwa hasa kipindi cha kwanza ambapo Nicolas Jackson alipiga mpira uliogonga mwamba na Ismaila Sarr kukosa nafasi ya wazi ya kufunga.