Infantino Aeleza Sababu ya Mwamuzi wa Somalia Kuzuiwa Marekani

Rais wa Shirikisho la Soka Duniani (FIFA), Gianni Infantino, amesema ni jambo la kusikitisha kwa mwamuzi wa Somalia, Omar Artan, kunyimwa ruhusa ya kuingia nchini Marekani licha ya kuwa alikuwa amepangiwa kushiriki katika michuano ya Kombe la Dunia.

Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari kabla ya kuanza kwa mashindano hayo, Infantino alisema FIFA imeguswa na kilichomtokea Artan, lakini haiwezi kudhibiti maamuzi ya serikali kuhusu masuala ya uhamiaji na usalama.

“Ni jambo la kusikitisha kilichomtokea Omar, mwamuzi kutoka Somalia. Tunajaribu kila wakati kutafuta suluhisho, lakini hatuwezi kuamuru serikali au vyombo vya usalama kuhusu nani aingie au asiruhusiwe kuingia nchini,” alisema Infantino.

Artan, ambaye alichaguliwa kuwa mwamuzi bora wa kiume barani Afrika mwaka jana, alidai kuwa alikuwa na viza halali ya kuingia Marekani. Hata hivyo, alizuiwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Miami na baadaye kurejeshwa nchini Uturuki.

Kwa mujibu wa afisa wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani, mwamuzi huyo alihusishwa na watu wanaoshukiwa kuwa wanachama wa makundi ya kigaidi, jambo lililomfanya akose sifa za kuruhusiwa kuingia nchini humo.

Iwapo angeruhusiwa kushiriki, Artan angekuwa mwamuzi wa kwanza kutoka Somalia kuchezesha mechi katika fainali za Kombe la Dunia.

Infantino pia aliulizwa kuhusu taarifa za Marekani kuwanyima viza baadhi ya maafisa wa timu ya Iran, ambapo alisisitiza kuwa FIFA haiwezi kuingilia mamlaka ya serikali kuhusu nani anaruhusiwa kuingia nchini.

“FIFA ni taasisi ya michezo, si serikali ya dunia. Tunafanya kazi kuhakikisha mashindano yanafanyika vizuri, lakini masuala ya usalama na uhamiaji yanabaki chini ya mamlaka ya nchi husika,” alisema.

Aidha, Infantino aliwataka wadau wa michezo kuwa watulivu huku akisisitiza kuwa FIFA inaendelea kushughulikia changamoto zinazojitokeza kabla na wakati wa mashindano.

“Tunafanya kazi. Dunia ya sasa ina changamoto nyingi za kiusalama, na mara nyingi usalama hupewa kipaumbele kuliko jambo lolote,” aliongeza.