Fainali ya CAFCC Kutimua Vumbi Cairo Usiku wa Leo

Pazia la michuano ya CAF Confederation Cup msimu wa 2025/26 linafungwa rasmi leo Mei 16, 2026, kwa mchezo wa mkondo wa pili wa fainali utakaopigwa katika dimba la Cairo International Stadium nchini Misri.

Mchezo huo unawakutanisha wenyeji Zamalek SC dhidi ya USM Alger, katika pambano la kusisimua litakaloanza majira ya saa 3:00 usiku.

Huu ni mchezo wa pili wa fainali ambapo USM Alger wanaingia wakiwa na faida ya bao 1-0 baada ya kushinda mchezo wa kwanza, hali inayoongeza presha kubwa kwa Zamalek SC ambao wanacheza mbele ya mashabiki wao.

Timu hizi zote mbili zina historia kubwa kwenye michuano hii, ambapo USM Alger walitwaa ubingwa msimu wa 2022/23 dhidi ya Yanga SC, kabla ya Zamalek SC nao kutwaa taji hilo msimu uliofuata dhidi ya RS Berkane.

Zamalek SC wanatafuta kutwaa ubingwa wa tatu wa michuano hiyo, huku USM Alger wakisaka taji la pili katika historia yao, jambo linalofanya fainali hii kuwa na mvuto mkubwa zaidi.

Mashabiki wa soka barani Afrika wanatarajiwa kushuhudia mchezo mkali wenye mbinu, kasi na presha kubwa, huku kila timu ikisaka kuandika historia mpya katika soka la Afrika.