Rais Samia Apewa Tuzo na BMT Kutambua Mchango Wake Kwenye Michezo

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda amekabidhi Tuzo Maalum ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa Waziri Mkuu, Mwigulu Lameck Nchemba, ikiwa ni kutambua mchango mkubwa wa Rais huyo katika maendeleo ya sekta ya michezo nchini.

Makabidhiano hayo yamefanyika katika hafla ya Tuzo za Baraza la Michezo la Taifa (BMT) 2025 zilizofanyika katika Ukumbi wa The Super Dome Masaki jijini Dar es Salaam, ambapo wadau mbalimbali wa michezo walihudhuria kushuhudia tukio hilo la heshima.

Tuzo hiyo maalum imetolewa kama ishara ya kutambua juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan katika kuimarisha na kuwekeza katika sekta ya michezo, hatua ambayo imechangia kwa kiasi kikubwa ukuaji wa ushindani na mafanikio ya wanamichezo wa Tanzania ndani na nje ya nchi.

Katika hafla hiyo, viongozi mbalimbali wa serikali, wanamichezo na wadau wa michezo wameendelea kusisitiza umuhimu wa kuendeleza mafanikio yaliyopatikana kupitia uwekezaji na sera zilizowekwa na Serikali ya Awamu ya Sita katika sekta ya michezo.