FIFA Yathibitisha Ushiriki wa Iran Kombe la Dunia 2026 Licha ya Mvutano wa Kisiasa

Rais wa Shirikisho la Soka Ulimwenguni, (FIFA), Gianni Infantino amethitibitisha kuwa Iran itashiriki mashindano ya Kombe la Dunia 2026 inayotarajiwa kuanza Juni 11 hadi Julai 19, 2026 licha ya mvutano kijiografia na kisiasa baina ya Marekani, Israel na Iran.

Akizungumza kwenye Mkutano wa 76 wa FIFA huko Vancouver mnamo Aprili 30, 2026, Infantino alisema bila shaka, Iran itashiriki Kombe la Dunia la FIFA 2026 linaloandaliwa kwa ushirikiano kati ya Marekani, Canada na Mexico na kubainisha kwamba hakuna wasiwasi wowote kwamba Iran itacheza kwenye ardhi ya Marekani.

Hatua hiyo inakuja wakati kukiwa na wasiwasi kutokana na mvutano baina ya mataifa hayo huko Mashariki ya Kati huku Iran ikiripotiwa kuomba mechi zao kuchezewa Mexico badala ya Marekani lakini FIFA imetupilia mbali pendekezo hilo ikisisitiza kwamba mashindano hayo ni jukwaa la kuwaleta watu pamoja.

Kauli ya Infantino imefuatiwa na uungwaji mkono kutoka kwa Rais wa Marekani, Donald Trump ambaye amesema hata shida na ushiriki wa Iran kwenye michuano hiyo licha ya hapo awali mjumbe wake maalum Paolo Zampolli kupendekeza Italia ichukue nafasi ya Iran katika mashindano hayo.