Nyota wa FC Barcelona, Raphinha, ameomba radhi kufuatia ishara aliyofanya kuelekea mashabiki wa Atlético Madrid baada ya timu yake kutolewa katika hatua ya robo fainali ya UEFA Champions League.
Raphinha, ambaye hakushiriki kwenye mchezo wa marudiano kutokana na majeraha ya paja, alionekana akijibu mashabiki wa Atlético akiwa uwanjani baada ya mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa Metropolitano. Inaripotiwa kuwa alifanya ishara iliyodhaniwa kumaanisha kuwa wapinzani wameondolewa, jambo lililozua malalamiko na huenda likamfanya achukuliwe hatua na UEFA.
Baadaye, nyota huyo wa Brazil aliomba radhi kupitia chapisho alilolitoa akieleza kuwa kitendo hicho kilitokana na hasira za muda mfupi na hakionyeshi tabia au maadili yake halisi.
“Naomba radhi kwa ishara yangu, ambayo haiakisi maadili au tabia yangu. Ilitokea katika wakati wa hisia kali, kutokana na shabiki aliyekuwa akinidhalilisha,” alisema Raphinha.
Hata hivyo, Raphinha pia alikosoa vikali uamuzi wa waamuzi baada ya mechi hiyo, akidai kuwa Barcelona ilidhulumiwa katika michezo yote miwili ya hatua hiyo ya mtoano.
Kauli zake ziliungwa mkono na baadhi ya wachezaji wa Barcelona, ambao nao walionesha kutoridhishwa na maamuzi ya waamuzi, huku viongozi wa klabu wakisema watawasilisha malalamiko rasmi kwa UEFA.
Kwa upande wa Atlético Madrid, kipa wao Juan Musso alikanusha madai ya “udhulumu,” akisisitiza kuwa matokeo yalipatikana uwanjani kwa mujibu wa mchezo.
Atlético Madrid waliifunga Barcelona jumla ya mabao 3-2 baada ya mechi mbili, na kufuzu kwenda hatua ya nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa.