Dabi ya Kariakoo Kuhamia Zanzibar Rasmi – TPLB Yafafanua Sababu

Afisa Habari wa Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB), Karim Boimanda, ameeleza sababu za kuhamishwa kwa mchezo wa Dabi ya Kariakoo uliopangwa kupigwa Machi 01, 2026.

Kwa mujibu wa Boimanda, dabi hiyo kati ya Yanga SC (wenyeji) dhidi ya Simba SC sasa itapigwa katika Uwanja wa New Amaan Complex badala ya Benjamin Mkapa Stadium kama ilivyopangwa awali.

Boimanda amesema uamuzi huo umefanywa kwa kuzingatia kuwa Machi 1, 2026, Uwanja wa Benjamin Mkapa utakuwa na matumizi mengine — ukitarajiwa kuwa mwenyeji wa mashindano makubwa ya Kimataifa ya Qur’an yatakayoshirikisha mabara yote ya dunia.

Katika tukio hilo, mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Hussein Mwinyi.

Amesisitiza kuwa kanuni za ligi zinaruhusu kubadilisha uwanja endapo kutakuwa na sababu za msingi za kiusalama au kiutendaji, hivyo hatua hiyo imechukuliwa kwa mujibu wa taratibu.

Uhamisho huo unatarajiwa kuongeza hamasa visiwani Zanzibar, huku mashabiki wa timu zote mbili wakitarajiwa kusafiri kwa wingi kushuhudia pambano hilo kubwa linalotikisa soka la Tanzania kila msimu.

Dabi ya Kariakoo ni moja ya mechi zenye mvuto mkubwa Afrika Mashariki, na mara zote huambatana na ushindani mkali ndani na nje ya uwanja.