MAKAMU Mwenyekiti wa Yanga, Frederick Mwakalebela amefunguka kuwa suala la mshambuliaji wa Zanaco, Moses Phiri kujiunga na timu hiyo kwa kusema ni suala la muda kwa kuwa linashughulikiwa kwa weledi mzuri.
Yanga inapambana kunasa saini ya mshambuliaji huyo aliyefunga mabao 17 msimu uliopita katika Ligi Kuu ya Zambia.
Habari zinaeleza kuwa Yanga ipo kwenye mazungumzo na mshambuliaji huyo ili kuweza kumuongeza kwenye kikosi hicho kwa ajili ya kufikia malengo ya timu hiyo ikiwa ni pamoja na kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara.
Mwakalebela amesema kuwa suala la mshambuliaji huyo kujiunga na timu hiyo ni jambo la muda kwa kuwa linafanywa kwa waledi mkubwa na viongozi wa timu hiyo.
“Usajili wa Phiri, upo katika mchakato mzuri kwa sababu tumefikia katika wakati mzuri ambao naamini utakamilika kwa kuwa upo chini ya watu makini ambao wanasimamia suala hilo.
“Sisi hatutaki kuwa waongeaji, nadhani mashabiki wenyewe wamekuwa wakijua namna tunavyofanya mambo yetu ingawa kwa sasa bado tunapambana kupata winga mwingine kutokana na wingi wa mejeruhi waliopo kwenye kikosi chetu,” amesema Mwakalebela.