SALAH,MANE WAPO KWENYE ULE UTATU WA KAZI CHAFU

MOHAMED Salah, raia wa Misri anayekipiga ndani ya Liverpool anaongoza ule utatu wa kazi chafu za kuwatungua makipa katika kikosi hicho kinachonolewa na Kocha Mkuu, Jurgen Klopp ambapo wengine wakorofi kwa kucheka na nyavu ni Sadio Mane na Roberto Firmino katika Ligi Kuu England.

Nyota huyo ambaye ni mkali wa kucheka na nyavu kibindoni kwa sasa ametupia jumla ya mabao 7 katika mechi 8 ambazo amecheza na ametengeneza nafasi nne za mabao.

Ni mashuti 33 ambayo amepiga Salah huku akiwa amekosa kufunga katika nafasi nne za wazi na ameotea mara tano. Mguu wake wenye nguvu ni ule wa kushoto ambapo amewatungua makipa mara sita huku ule wa kulia ukifunga bao moja pekee.

Nyota wa pili ni Sadio Mane ambaye huyu ni raia wa Senegal yeye ametupia mabao matano na hajatoa pasi ya bao kwa wakati huu katika mechi 8 ambazo amecheza ambapo ni mashuti 30 amepiga.

Mane ni mbaya kwa kutumia mguu wa kulia ambao ameutumia kuwapa tabu makipa katika mabao yake yote matano ambayo yapo kibindoni mwake kwa sasa ndani ya Ligi Kuu England.

Yule wa tatu anaitwa Robert Firmino mwamba mmoja hivi ambaye anatabasamu baya kwa makipa pale anapowatungua ila linapendeza kwa mashabiki wake wa Liverpool pamoja na wachezaji wenzake.

Ametupia mabao manne na mguu anaopenda kuutumia ni ule wa kulia ambao umetupia mabao matatu na ule wa kushoto umetupia bao moja pekee ndani ya ligi hiyo inayotajwa kuwa ngumu na pendwa duniani.

Vijana hao wa Klopp, Oktoba 24 wanakibarua cha kusaka ushindi katika mchezo wa Ligi Kuu England dhidi ya Manchester United inayonolewa na Kocha Mkuu, Ole Gunnar Solskjaer itakuwa katika Uwanja wa Old Trafford.