HELLO NOVEMBA, MKIA UTAKATIKA AMA NUSUNUSU KUYEYUKA

YAPO mengi yanayoongeza kasi na nguvu kwenye utendaji ikiwa ni pamoja na uhakika wa kuanza kesho ukiwa na tabasamu baada ya kumaliza kazi ya kula ng’ombe mzima aliyekuwa msumbufu.

Ajabu ni kwamba kuna waliomaliza ng’ombe na kazi ya kumaliza mkia ikawa ni kivumbi. Hapa tunakuletea baadhi ya nyota ndani ya Simba na Yanga ambao wanasubiri kuona kama mkia utakatika ama nusunusu ya kusugua benchi itatayeyuka namna hii:-

Ayoub Lakred

Alitambulishwa ndani ya Simba kuwa mbadala wa mwamba Aishi Manula ambaye alipata maumivu ya nyonga yaliyomuweka nje kwa muda mrefu. Kivumbi kilianza kwenye mechi mbili za Ligi ya Mabingwa Afrika katunguliwa nje ndani.

Power Dynamos walimtungua mabao matatu na kacheza mchezo mmoja wa ligi dhidi ya Coastal Union alipokamilisha dakika 90 bila kufungwa. Nafasi kikosi cha kwanza ni nusunusu inapotea huku Manula akianza kurejea kwenye ubora wake.

Tusubiri na tuone Novemba 5 kwenye Kariakoo Dabi mkia utakatika wa kusugua benchi ama itaendelea kuwa nusunusu kwake kuendelea kusugua benchi.

Luis Miquissone

Aliposepa 2021 na kuibukia Al Ahly aliandika rekodi ya kutoa hat trick ya pasi za mabao kwenye mchezo dhidi ya Gwambina, Uwanja wa Mkapa. Alitoa jumla ya pasi tisa za mabao akiwa kwenye ubora wake.

Karejea kwa mara nyingine ni nusunusu kuanza kikosi cha kwanza kwenye mechi za ligi licha ya kutoa pasi tatu za mabao. Novemba sasa inaanza kutakuwa na utofauti ama ataishi maisha yaleyale ya jana.

Moses Phiri

Ana zali na nyavu licha ya mabao yake yote aliyofunga kuanzia benchi. Mabao matatu kambani kawatungua Dodoma Jiji, Singida Fountain Gate na Ihefu.

Idd Chilunda

Ingizo jipya akiwa ni huru kutoka kwa matajiri wa Dar, Azam FC. Kapata zali la kucheza mechi mbili kati ya sita akikomba dakika 17 hajafunga wala kutoa pasi ya bao.

John Bocco

Uwezo wake hauchuji akiwa ni nahodha maisha yake ndani ya Simba yana furaha lakini hajapata zali la kuwatungua watani zake wa jadi Yanga kwenye mechi za ligi baada ya kujiunga na Simba.

Ni nusunusu furaha kwake kwa sasa itakamilika kama atapata bahati ya kuwafunga watani zake ila uhakika wa kuanza bado ni tatizo.

David Kameta

Upande anaocheza yupo mwamba Shomari Kapombe chaguo la kwanza la Roberto Oliveira. Novemba inaanza hajapata zali la kucheza mchezo hata mmoja kwenye ligi.

Aboutwalib Mshery

Kutoka Mtibwa Sugar na sasa ni ndani ya Yanga. Kutokuwa fiti kwa muda msimu wa 2022/23 kuliongeza ugumu kuwa shuhuda wengine wakicheza na sasa karejea kwenye ubora wake.

Zawad Mauya

Kiungo mkabaji mzawa mgumu ndani ya kikosi cha Yanga. Ni mechi nne kacheza kati ya saba akikomba dakika 192.

Farid Mussa

Nyakati zinakwenda kasi, nyota huyu kakomba dakika 26 kwenye mchezo mmoja wa ligi ndani ya Yanga.

Kibwana Shomari

Kazini kwake kuna kazi, uwepo wa Yao Attohoula kinara wa pasi za mwisho akiwa nazo nne unapunguza ile nusu ya imani kwamba anaweza kuanza kikosi cha kwanza Kariakoo Dabi. Kwenye mpira yote yanawezekana kwani uwezo wake Kibwana sio haba.

Crispin Ngushi

Mshambuliaji aliyewika akiwa na Mbeya Kwanza huko alikuwa ana uhakika wa kumaliza mkia mzima kikosi cha kwanza. Maisha yake ndani ya Yanga ni nusunusu akiishia kuwa shuhuda Kennedy Musonda, Clement Mzize wakipenya kikosi cha kwanza.

Jonas Mkude

Legend mwenye uzoefu na Kariakoo Dabi alipoanza kuonyesha uwezo wake akiwa na Simba. Yupo ndani ya Yanga kwa sasa bado hajajenga utawala wake kwenye eneo la kiungo taratibu anazidi kujitafuta.

Hafiz Konkoni

Mbeba mikoba ya Fiston Mayele, kibindoni ana bao moja. Ni nusunusu kwake kuanza Novemba 5 inawezekana mkia ukaisha akaonyesha uwezo wake.

Imeandikwa na Lunyamadzo Mlyuka na kutoka kwenye gazeti la Spoti Xtra.