Familia, marafiki, wachezaji wenzake na viongozi mbalimbali wa soka nchini Hispania wamekusanyika Alhamisi, Novemba 5, 2026, katika mazishi ya mshambuliaji wa klabu ya CD Tenerife, Jesús de Miguel, aliyefariki dunia baada ya kupata matatizo ya moyo kufuatia kugongana na kipa wa FC Andorra, Jesús Owono, wakati wa mchezo wa Ligi Daraja la Pili nchini humo.
De Miguel, mwenye umri wa miaka 30, alipata ajali hiyo dakika ya 96 ya mchezo uliochezwa Jumatatu, Novemba 2, 2026. Baada ya kugongana na Owono, alipata matatizo ya kiafya na kukimbizwa hospitalini kwa matibabu, hata hivyo alifariki dunia Jumanne, Novemba 3, licha ya juhudi za madaktari kuokoa maisha yake.
Mazishi ya nyota huyo wa soka yamefanyika katika mji wa Navahermosa, uliopo katikati mwa Hispania, ambao una wakazi takribani 3,000 na pia ni eneo linalohusishwa na asili ya familia yake.
Miongoni mwa viongozi mashuhuri waliohudhuria mazishi hayo ni Kocha wa timu ya taifa ya Hispania, Luis de la Fuente, Rais wa Real Madrid, Florentino Pérez, pamoja na Rais wa Shirikisho la Soka la Hispania, Rafael Louzán. Pia walikuwepo wachezaji na viongozi wa klabu ya CD Tenerife.
Akizungumza wakati wa mazishi hayo, De la Fuente amesema wamekusanyika kutoa pole na heshima kwa familia ya marehemu, akisisitiza umuhimu wa jumuiya ya soka kuungana wakati wa kipindi kigumu cha majonzi.
Familia ya De Miguel nayo imetoa shukrani kwa wote waliojitokeza na kuonesha mshikamano, ikieleza kuwa kifo chake kimeacha pengo kubwa lisiloweza kuzibika pamoja na kumbukumbu nyingi kwa watu waliokuwa karibu naye.
Kutokana na msiba huo, mamlaka za mji wa Navahermosa zimetangaza siku tatu za maombolezo, huku bendera zikipepea nusu mlingoti kuonesha heshima kwa marehemu.
Aidha, michezo iliyokuwa ikitarajiwa kuzikutanisha CD Tenerife dhidi ya Granada na FC Andorra dhidi ya Mallorca imeahirishwa kutokana na tukio hilo.
Katika hatua nyingine, mechi mbalimbali za soka nchini Hispania zimepangiwa kusimama kwa muda katika dakika ya tisa kumuenzi De Miguel, ambaye alikuwa akitumia jezi namba tisa.
Wakati huo huo, Jeshi la Polisi nchini Hispania limeanzisha uchunguzi ili kubaini mazingira yaliyozunguka kifo cha mshambuliaji huyo.
Kifo cha Jesús de Miguel kimeacha simanzi kubwa katika familia yake na jumuiya ya soka nchini Hispania, huku wachezaji, viongozi na mashabiki wakiendelea kutoa heshima kwa maisha na mchango wake katika mchezo huo.