GAMONDI AJA NA MPANGO KAZI WA KUVURUGAVURUGA

MIGUEL Gamondi Kocha Mkuu wa Yanga amevuruga ramani za wapinzani wao wanaofikiria mbinu yake ya kupata mabao itakuwa kwa washambuliaji wanaonza kikosi cha kwanza ikiwa ni Clement Mzize na Kenedy Musonda.

Mrithi huyo wa mikoba ya Nasreddine Nabi ameibuka na mbinu mpya kwenye upande wa ushambuliaji tofauti na Nabi ambaye alikuwa akimtumia Fiston Mayele eneo la utupiaji misimu miwili mfululizo.

Gamondi amesema kuwa kinachofanyika kwa sasa ni timu nzima kutafuta matokeo ya ushindi bila kujali nani ambaye atapata nafasi ya kufunga kwenye mchezo husika.

“Ikiwa utakuwa unawategemea washambuliaji peke yake inakuwa rahisi kwa wapinzani kuwapa presha hao wachezaji hao ambao mwisho watakwama kukupa ushindi hivyo wanacheza wakiwa ni timu.

“Kila mchezaji anafunga awe ni beki, kiungo na hata washambuliaji nao wanafunga jambo ambalo ni zuri kwetu. Makosa tunayafanyia kazi ili kuwa imara kwa wakati ujao kwa kuwa mechi ni nyingi na ushindani ni mkubwa,” amesema Gamondi.