MAKUNDI UEFA NI KAZIKAZI, ARSENAL VIBONDE

KIU ya mashabiki wa soka ya kutaka kujua nani atapangwa na nani kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya (Uefa) ilifika mwisho baada ya juzi Alhamisi makundi hayo kupangwa huku Manchester United wakipangwa kundi moja na mabingwa wa Ujerumani, Bayern Munich.

Vijana hao wa kocha Eric ten Hag, Man United wamepangwa kwenye kundi A la michuano hiyo wakiwa na Bayern ambayo anaichezea straika Harry Kane sambamba na Copenhagen ya Denmark na Galatasaray ya Uturuki.

Wakati United wakipangwa kwenye kundi A, wapinzani wao wa karibu, Arsenal wao wamepangwa kwenye kundi B ambalo linajumuisha timu za Sevilla ya Hispania, PSV Eindhoven ya Uholanzi na RC Lens ya Ufaransa.

Kundi hilo linaonekana kuwa rahisi zaidi kwa Arsenal ambao wanafundishwa na kocha Mikel Arteta huku wakiwa wanapewa nafasi kubwa ya kusonga mbele.

Mabingwa watetezi wa kombe hilo, Manchester City wao wamepangwa kundi G wakiwa na timu za RB Leipzig ya Ujerumani, Red Star Belgrade na Young Boys, kundi ambalo City anapewa nafasi kubwa ya kuongoza kundi hilo.

Wageni wa michuano hiyo, Newcastle United ambao walimaliza ndani ya nne bora ya Premier msimu uliopita wao wamepangwa kwenye kundi la kifo, kundi F ambalo linazijumuisha timu za Paris Saint-Germain ya Ufaransa, Borussia Dortmund ya Ujerumani na AC Milan ya Italia.